Fashion Association of Tanzania(FAT) waungana na serikali mapambano dhidi ya maambukizi Covid-19


•    Wabunifu waonyesha kwa vitendo mapigano dhidi ya maambukizi ya Covid-19

Fashion Association of Tanzania (FAT) chaendesha mchakato wa uchangiaji wa vitakasa ikiwa sehemu ya mchango wao dhidi ya maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na kirusi cha Corona (Covid-19).

Jumla ya wabunifu, wanamitindo na wadau wa sekta hiyo 66, wameweza kuchangia katoni 80 (sawa na lita 1,600) za vitakasa, katoni 60 kati ya hizo zikiwa ni “lit lavender disinfectant” na 20 zikiwa ni “zap bleach regular” vyenye thamani ya Sh. Milioni mbili za Kitanzania (Tsh. 2,000,000).

Wanachama wa “Fashion Association of Tanzania” pamoja na wadau wengine wa tasnia hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho Ndg. Mustafa Hassanali, walikabidhi vitakasa hivyo kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania Bi. Angelina Ngalula kwenye ofisi za taasisi ya kitaifa ya utafiti wa matibabu (NIMR).

Ndugu Hassanali alimshukuru Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kutenga muda wake kupokea mchango wao, na aliwashukuru pia wabunifu, wanamitindo na wadau wote wenye mapenzi mema na Tanzania kwa michango na kujitoa kwao katika kuhakikisha upatikanaji wa vitakasa hivyo kama sehemu ya mapambano dhidi ya maambukizi ya homa ya mapafu inayosababishwa na kirusi cha Corona (Covid – 19).

Sambamba na hilo wabinifu hao kwa pamoja wametoa rai kwa Watanzania wote kulichukulia kwa uzito swala hilo kwani ni hatari endapo hatua stahiki hazitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufwata ushauri unaotolewa na watalaam wa afya juu ya mapambano dhidi ya ugonjwa huu.

Imetolewa na Fashion Association of Tanzania.






No comments: