DKT KAWAMBWA ACHANGIA MISAADA KUPAMBANA NA CORONA






……………………………………………………………………………..
NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO 

Mbunge wa jimbo la Bagamoyo mkoani Pwani Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa, amegawa ndoo za maji kwaajili ya kunawa mikono, pamoja na sabuni katika maeneo mbalimbali ya kata ya Dunda, Nianjema na Magomeni ikiwa ni muendelezo wa mapambano dhidi ya maamukizi ya ugonjwa wa Corona. 

Ziara hiyo iliyopitia vijiwe mbalimbali vya pikipiki na maeneo ya masoko, Dkt. Kawambwa aliwatahadharisha wafanyabiashara na watu wanaokuja katika maeneo hayo kupata mahitaji mbalimbali kuwa ugonjwa wa Corona ni hatari kwani unaenea kwa kasi hivyo hakuna budi kuchukua tahadhari na maradhi hayo. 

Aidha, Dkt. Kawambwa aliwataka waendesha pikipiki kuhakikisha abiria zao wananawa vizuri mikono yao kwa kutumia maji tiririka na sabuni hizo kabla ya kupanda kwenye usafiri huo, kwani kwa kufanya hivyo kwa kiasi kikubwa watajiepusha na maambukizi hayo. 

“Vijana wangu waendesha pikipiki na wafanyabiahara hakikisheni mnachukua tahadhari kwa kiasi kikubwa kuhusu ugonjwa huu ili uweze kujikinga wewe binafsi na familia nyumbani” alisema Dkt. Kawambwa. 

“Tunaona namna ambavyo maambukizi hayo yanavyoendelea siku hadi siku kwa nini nawe usiunge mkono juhudi za muheshimiwa Rais Dkt. Maghufuli na viongozi mbalimbali za kuhakikisha tunabaki salama”? alihoji. 

Alisema ameongea na wahisani waliowahi pia kusaidia katika operesheni ya macho bure ambao ni Bilal eye camp, nao kwa kuona umuhimu wa tahadhari ambapo wamekubali kutoa ndoo za maji na sabuni ili zitumike kunawa mikono. 

Kwa upande wao madiwani wa viti maalum, Shumina Rashidi na Afsa Kilingo waliwataka wafanyabiashara hao wa kata hizo kushirikiana na serikali katika kuhakikisha wanashinda vita dhidi ya corona. 

Aidha, madiwani wa kata ya Nianjema Abdul Pyallah na Diwani wa kata Dunda Dickson Makamba walimshukuru na kumpongeza Mbunge Dkt. Kawambwa, kwa kufanikisha zoezi hilo muhimu. 

Kwa upande wao waliopokea misaada hiyo ya ndoo za maji na sabuni kwaajili ya kunawa mikoni wamemshukuru Mbunge huyo kwa juhudi zake za kuwajili wananchi wake hasa katika kipindi hiki cha ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona.

No comments: