Dkt. Kalemani: Lipieni tujue idadi ya wateja tusambaze nguzo tuwawashie umeme!
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ( kulia) akiwasha umeme katika Kijiji cha Bugwego Kata ya Bwongera, wilayani Chato mkoani Geita alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji umeme vijijini katika maeneo hayo, Mei 18,2020.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani(kushoto),akizungumza na mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Rusungwa Kata ya Nyamirembe,Wilayani Chato,mkoani Geita baada ya kuwasha umeme katika nyumba yake alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji umeme vijijini katika maeneo hayo, Mei 18,2020.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani,( kushoto) akiruka maji wakati akienda kukagua maendeleo ya usambazaji wa umeme vijijini katika Kijiji cha Bugwego Kata ya Bwongera Wilayani Chato,mkoani Geita, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji umeme vijijini katika maeneo hayo, Mei 18,2020. Dkt. Kalemani alilazimika kutembea kwa mguu kufikia maeneo hayo kuwa magari hayafiki kwa sababu ya kuharibika kwa barabara kufuatia mvua kubwa zilizokuwa zinanyesha katika maeneo mbalimbali nchini.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ( katikati) akiwasha umeme katika Kata ya Businda wilayani Bukombe mkoani Geita alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji umeme vijijini katika maeneo hayo, Mei 18,2020.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ( kulia) akizungumza na wakazi wa Kata ya Businda wilayani Bukombe mkoani Geita(hawapo pichani) alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji umeme vijijini katika maeneo hayo, Mei 18,2020.
Na Zuena Msuya Geita,
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewaambia wanakijiji ambao umeme ushafika katika maeneo yao walipie gharama za kuwashiwa umeme ili kufahamu idadi ya wateja, nguzo zisambazwe na kuunganishwa kulingana na wateja waliopo kwa wakati husika.
Dkt. Kalemani alisema hayo wakati akiwasha umeme katika Kijiji cha Rusungwa Kata ya Nyamirembe, Bugwego Kata ya Bwongera Wilayani Chato na Kijiji cha Businda Wilayani Bukombe mkoani Geita alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji umeme vijijini katika maeneo hayo, Mei 18,2020.
Dkt. Kalemani alisema kuwa vijiji vingi tayari vimefikiwa na umeme katika maeneo machache hivyo wananchi wanatakiwa kulipia gharama za kuwashiwa umeme ili ifahamike idadi ya wateja waliopo na kupelekewa nguzo za kusambazwa kwa wateja waliopo na wawashiwe umeme.
Pia alieleza kuwa kitendo cha wanakijiji kuacha kulipia gharama za kuuwashiwa umeme wakisubiri kuona nguzo zimesambaa katika maeneo yao, hali ya kuwa tayari umeme umeshafika katika vijiji vyao, kunachelewesha kasi ya kuwawashia umeme wanakijiji katika nyumba zao kwa kuwa mamlaka husika zinasambaza nguzo kulingana na wateja waliopo eneo husika kwa wakati husika, hivyo wananchi wachangamkie fursa na kulipia gharama ya shilingi 27,000 tu.
Vilevile alisema kuwa wanakijiji hao hawapaswi kuhoji kuhusu nguzo kufika katika maeneo yao kwakuwa hilo si jukumu lao, ila wanachotakiwa kufanya ni kulipia gharama za kuwashiwa umeme tu, na baada ya kulipia gharama ndipo wahoji endapo hawajawashiwa umeme.
"Kijiji chochote ambacho umeme umeshafika na kuunganishwa, hata kama umewashwa katika nyumba moja, wanakijiji sasa jukumu lenu ni kulipia gharama kuwashiwa umeme ili ijulikane idadi ya wateja waliopo na mletewe nguzo na kuungwa, nguzo zinaletwa na kusambazwa kulingana na idadi ya wateja waliopo,kwa wakati husika ili wote wanaotaka kwa wakati huo wapate, msihoji kuwa nguzo zinafika lini hilo si jukumu lenu! Ninyi mnapaswa kuhoji lini mtawashiwa umeme mkiwa tayari mmelipia gharama, na hapo tutachukua hatua kwa yeyote atakayechelewa kumuwashia umeme mteja aliyekwisha lipia gharama za uunganishaji, Sasa lipieni msisubiri nguzo ”, Alisema Dkt. Kalemani
Aidha Dkt. Kalemani alirejea kusema kuwa mkandarasi yeyote atakayeshindwa kumaliza kazi ya usambazaji wa umeme vijijini kwa mujibu wa mkataba,atashitakiwa kisheria kwa kosa la kuwacheleweshea wananchi huduma pamoja na kukatwa asilimia 10 ya malipo yake yaliyosalia.
Aidha kazi hiyo atapewa mkandarasi mwingine amalizie na hiyo asilimia 10 iliyokatwa ndiyo itatumika kumlipa mkandarsi atakayekabidhiwa jukumu la kumalizia kazi hiyo.
Aliendelea kuwasisitiza wakandarasi walio nyuma ya muda katika kukamisha kazi hizo kuongea nguvu kazi katika maeneo ya kazi ili wasikumbane na kadhia hivyo.
Vilevile alitoa wiki moja kwa mkandarasi kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania( TANESCO) kuwawashia umeme wakazi wa Mtaa wa Businda waliokwisha lipia gharama hizo na kukumuagiza Mkuu wa Wilaya ya Bukombe kumchukulia hatua mkandarasi wa eneo hilo endapo atashindwa kufanya hivyo.
Dkt.Kalemani alisema kuwa mkandarasi yeyote ambaye hakufanya vizuri katika utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa umeme vijijini (REA), hatapewa nafasi ya kufanya kazi katika miradi inayokuja hata kama ameshinda vigezo vya Zabuni.
"Mkuu wa Wilaya nakukabidhi mkandarasi huyu akishindwa kuwauwashia umeme wanakijiji hao waliolipia gharama pamoja na kuwaunganishia wale aliowapita pale, mchukulie hatua ikiwezekana muweke korokoroni, hii iwe fundisho kwa wakandarasi wengine nchini kwa sababu wengi wanachewa kuwawashia wananchi umeme wakati tayati wamelipia, na utaratibu ni ndani ya siku saba baada ya mwananchi kulipia awashiwe umeme sio kuwaacha tu bila kuwaeleza sababu yoyote", Alisisitiza Dkt. Kalemani.
Pia aliwawasisitiza mameneja wa TANESCO kote nchini kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza azma ya serikali ya kuunganisha umeme katika kijiji vyote nchini ifikapo 2021, pia wazingatie viwango na tathmini iliyowekwa katika kuwapima utendaji kazi wao.
Juni 30, 2020 wakandarasi wote nchini wanaotekeleza mradi wa usambazaji wa umeme vijijini wanatakiwa kukamilisha kazi hiyo kwa mujibu wa mkataba, hata hivyo serikali imekaririwa ikisemakuwa haitaongeza muda kwa yeyote ambaye atashindwa kukamilisha kazi hiyo na tachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
No comments: