COSTECH yamwezesha Mbunifu kutengeneza mashine inayoweza kupima magonjwa ya moyo

 Mbunifu wa mashine ya kupima magonjwa ya Moyo, Janeth Henry Tilya.
 Mbunifu Janeth Henry Tilya akionesha waandishi wa habari (hawako pichani)namna  mashine inavyofanya kazi.


Na COSTECH
TAKWIMU za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa kila mwaka wastani wa watu milioni 58 hupoteza maisha duniani kote. Vifo vya watu milioni 41 sawa na asilimia 71 ya vifo vyote kwa mwaka husababishwa na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo magonjwa ya moyo, kisukari, figo na shinikizo la damu.

Magonjwa ya moyo ndio yanayoongoza katika kusababisha vifo vingi. Inakadiliwa kuwa watu milioni 17 hupoteza maisha kila mwaka kwa magonjwa ya moyo. Kutokana na ukweli huo, Serikali chini ya Rais wa awamu ya Tano, Mheshimiwa Daktari John Pombe Magufuli ilizindua awamu ya pili ya mkakati wa miaka mitano (2016-2020) wa kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ili kupunguza vifo vitokanavyo na maradhi hayo (ambayo huchangia asilimia 27 ya vifo) nchini kila mwaka.

Ili kuchangia juhudi za serikali katika kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza Tume ya Taifa ya Sayansi (COSTECH) imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia watafiti na Wabunifu mbali mbali kuja na majibu ya kitafiti na ubunifu wa teknolojia zinazowezesha kupambana na magonjwa hayo. Katika Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu yaliyofanyika mwaka 2019 (MAKISATU 2019), Mbunifu Janeth Henry Tilya aliye buni mashine ya kupima magonjwa ya moyo hapa nchini aliibuliwa na kuwezeshwa.

Mashine hiyo inaweza kutumika kupima wagonjwa wakiwa maeneo mbali mbali na kutambua kama wana magonjwa ya moyo au la. Kupitia mashine hiyo mgonjwa anaweza kupimwa na taarifa za vipimo kutumwa kwa daktari kwa njia ya simu ya mkononi naye daktari anauwezo wa kumuandikia matibabu ya mgonjwa anayostahili kupatiwa. Kwa njia hiyo daktari na mgonjwa huwasiliana kwa njia ya kimtandao, vipimo vya mgonjwa na majibu ya vipimo vya mgonjwa huwafikia daktari na mgonjwa kwa njia ya mtandao. 


Mbunifu Janeth Henry Tilya akiongea na waandishi wa habari namna alivyoibuliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH na kuwezeshwa kuendeleza ubunifu wake.

Hii inarahisisha matibabu lakini pia inapunguza gharama ambazo mgonjwa hutumia kufuata matibabu hasa kwa wagonjwa wanaoishi mbali na hospitali au vituo cha afya. Mashine hii pia inasaidia kutatua changamoto za upungufu wa madaktari kwani daktari mmoja huweza kutibu wagonjwa wengi zaidi kupitia mashine hiyo kwa vile vipimo vya wagonjwa hupatikana kwa haraka na majibu kurudishwa kwa wajongwa kwa haraka zaidi.

 “Hii mashine inaweza kutumika nyumbani, zahanati au kituo cha afya na pengine popote ambako hakuna daktari wa magonjwa ya moyo. Mgonjwa aliye mbali anaweza kuwasiliana na daktari magonjwa ya moyo na daktari anaweza kumtibu mgonjwa bila kuonana,” anasema mbunifu Janeth.

Ubunifu wa Janeth ukiendelezwa sio tu unatoa mchango kwa jamii ya watanzania bali anaunga mkono juhudi za Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG) ya kuwa na huduma za afya kwa wote sambamba na mpango wa Serikali wa kuimarisha na kuboresha matibabu ya kibingwa nchini ili kuokoa maisha ya wananchi wengi na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Takwimu za Wizara ya afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto zinaonyesha kati ya Julai 2018 na Machi 2019 wagonjwa 62 walipewa rufaa ya kwenda kutibiwa nje wakilinganishwa na 114 waliokuwapo mwaka mmoja uliopita. 

Kwenye idadi hiyo, wagonjwa wa saratani (16) waliongoza wakifuatiwa na magonjwa ya moyo (15) halafu mifupa (12) mishipa ya fahamu (6), mishipa ya damu (5), figo mmoja na magonjwa mengine (7).

Janeth anapenda watu wengi zaidi watibiwe nchini na anaamini mashine hiyo ikizalishwa kwa wingi kulingana na mahitaji na kutumiwa na Watanzania, itasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na magonjwa ya moyo.

“Mimi nimeibuni, nikipata mwekezaji ikiwamo Serikali nitafurahi zaidi. Kwa sasa nakamilisha vitu vidogo vilivyobaki. Mwanzo ilikuwa inaweza kutumiwa na mtu mmoja ila nina iboresha iweze kutumika na watu wengi hata katika zahanati,” Janeth anasema.

Akielezea tofauti ya ubunifu wa kifaa au mashine aliyoibuni na mashine zinazotumiwa hospitalini ambazo hununuliwa kutoka kwa kampuni mbalimbali duniani, anasema mashine zilizoko hospitalini kwa sasa hutumika kupima mgonjwa mmoja akiwa na daktari au akiwa hospitalini, ila mashine aliyobuni inaweza kupima wagonjwa walio mbali na hospitali na kutuma taarifa kwa daktari kwa ajili ya matibabu kwa njia ya mtandao.

Ubunifu wa mashine ya kupima magonjwa ya moyo ulimfanya Janeth awe miongoni mwa zaidi ya wabunifu 50 walioibuka washindi wa Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Tekonolojia na Ubunifu (MAKISATU) yanayoratibiwa kila mwaka na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa ajili ya kuwaibua wabunifu na kuishauri Serikali namna ya kuwaendeleza wabunifu hao.

Kwa kupitia COSTECH, Janeth amepokea ruzuku ya kuendeleza ubunifu wake pamoja na kupata nafasi ya kutumia maabara za Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph ambako anapewa ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wahadhiri waliopo Chuoni hapo. Janeth pia anajengewa uwezo wa kupata hati miliki ili kulinda ubunifu wake, na jinsi ya kutafuta masoko na kuandaa mpango biashara kabla ya kuingiza ubunifu wake sokoni.
===


Mbunifu wa mashine ya kupima magonjwa ya moyo, Janeth Tilya akieleza jinsi inavyofanya kazi. Janeth ni mhitimu wa shahada ya uhandisi ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph.

No comments: