BOB MAKANI- MTANZANIA KIPANGA ALIYEKUWA NA TALANTA LUKUKI NA KUCHEZEA TIMU YA TAIFA YA UGANDA 'GOSSAGE CUP'.


By MZEE WA _ATIKALI  ✍️✍️✍️


1. Usuli

Bongolanders  walimjua marehemu BOB NYANGA  MAKANI kama Mwanasiasa mahiri. Lakini, wengi hawajui kwamba BOB alikuwa ni kipanga aliyejaaliwa talanta lukuki na alifanya mambo mengi ya kipekee na yasiyo mfanowe ikiwemo kuichezea Timu ya Taifa ya Uganda kwenye michuano ya "Gossage Cup" kabla ya Uhuru, licha ya kuwa Mtanzania!.

Hivyo, ATIKALI hii inammyambua marehemu BOB NYANGA MAKANI toka anazaliwa hadi umauti unamfika huku ikitanabaisha talanta zake hizo mujarab.

2. Kuzaliwa kwa BOB

BOB alizaliwa mwaka 1939 huko hospitali ya Kolandoto, Wilaya ya Kishapu, Shinyanga, baba yake akiitwa ALLY MAKANI @"Wakili" kutokana na kujua Lugha 7 ikiwemo Kiingereza na Kiarabu.

3. Elimu ya BOB

3.1 Elimu ya Msingi

Mwaka 1942 akiwa na miaka 6, BOB alianza masomo ya msingi katika shule ya msingi Ibadakuli iliyoko wilayani humo. Alikuwa kijana hodari sana darasani.

3.2 Elimu ya Sekondari

BOB alipohitimu elimu ya msingi alichaguliwa kujiunga na shule maarufu na iliyokuwa bora kuliko zote Tanganyika wakati huo ya "Tabora Boys" baada ya kufaulu vizuri mitihani yake.

4. BOB Awika Tabora Boys

4.1 BOB:- Mwanafunzi Kipanga

BOB alikuwa genius kwani tofauti na wanafunzi wenzake waliokuwa wanalazimika kukesha wakibundi, yeye alielewa darasani na hivyo alihitaji kusoma kidogo tu. Daima aliongoza darasani na mwisho wa kila temu alikuwa akisomba zawadi zote za masomo!.

4.2 BOB-: Mwanamichezo Hodari

4.2.1 BOB-: Bingwa wa Long Jump & High Jump

BOB alikuwa mwembamba mrefu hivyo michezo hii miwili aliimudu vilivyo huku akishikilia rekodi ya Taifa ya Long jump akiwa Mwanafunzi! Aidha, BOB alikuwa pia ni hodari sana wa kufukuza upepo!.

4.2.2 BOB-: Mwanasoka Hodari

BOB alichaguliwa timu ya mpira wa miguu ya shule mara tu alipojiunga ba Tabora Boys kutokana na kipaji chake cha kipekee cha gozi la ng'ombe!.

4.2.3 BOB Aichezea Tabora Michuano ya Sunlight Cup

BOB, licha ya kuwa Mwanafunzi, alichaguliwa timu ya mkoa wa Tabora kwenye michuano ya Sunlight Cup au Taifa Cup kutokana na kuupiga mpira mwingi michuano ambayo Tabora Boys ilikuwa ikishiriki mkoani Tabora. Marehemu MATHIAS KISSA ambaye mwaka 2000 alichaguliwa na TFF kuwa "Mwanasoka Bora wa Karne TZ" pia aliichezea Tabora  kwenye michuano hiyo ya Sunlight Cup akiwa mwanafunzi.

4.2.4 BOB & KISSA-: Vipenzi vya Headmaster Mzungu

 Headmaster wa shule wa Tabora Boys enzi hizo, mzungu Crabbe, aliwapenda sana BOB na KISSA kwa umahiri wao kwenye kabumbu uliopelekea kuiletea, mara kwa mara, heshma kubwa shule hiyo.

5. BOB Aenda Makerere University

5.1 BOB Apasua paper

BOB alifaulu vizuri sana mtihani wake wa mwisho Tabora Boys  na kuchaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda kusomea Uchumi.

5.2 BOB Aendeleza Ukipanga Makerere

BOB, alipojiunga Makerere, aliendelea kuwatimulia vumbi wanafunzi wenzake kimasomo na kufaulu vizuri sana mitihani yake.

5.3 BOB Akonga Nyoyo Michezoni

BOB alikuwa Mwanafunzi maarufu sana Makerere kutokana na ukipanga, wajihi wake na uhodari michezoni kwani talanta zake zliijiweka bayana.

5.3.1 BOB-: Mwanasoka Bora Makerere

Katika michuano mbalimbali ambayo Chuo cha Makerere kilishiriki, BOB alitia fora na bila ubishi akawa ndiye mwanasoka bora kabisa chuoni hapo.

6. KABAKA WA BAGANDA Ampangishia BOB Presidential Suite Hotel ya Kifahali

KABAKA wa BAGANDA ie Sir EDWARD FREDRICK WLLIAM DAVID WALUGEMBE MUTEBI LUWANGULA MUTEESA II, alivutiwa mno na uhodari wa BOB kwenye kabumbu. Hivyo, KABAKA akamtoa BOB bwenini Makerere na kumpangishia chumba maalum Presidential Suite kwenye hotel ya Grand Imperial Hotel iliyokuwa nzuri kuliko zote jijini Kampala enzi hizo. KABAKA akampatia BOB Coupon  ambapo BOB aliweza kula na kunywa chochote alichokitaka hotelini hapo bila kulipa!. BOB, kwa hakika, licha ya kuwa mwanafunzi,  akaishi maisha ya anasa sana!.

7. BOB Achaguliwa UGANDA CRANES

BOB alichaguliwa timu ya Taifa ya Uganda (Uganda Cranes) ambapo KABAKA alimwezesha kupata passport na hivyo akashiriki michuano ya Gossage Cup iliyoshirikisha Uganda, TG, Kenya na ZNZ.

Katika hali ya kustaajabisha,  Mtanzania BOB akawa anaichezea Uganda ambayo ilikuwa ikiionea mara kwa mara Tanganyika iliyokuwa chovu na kutwaa ubingwa mara lukuki wa Gossage Cup!.

8. BOB Ahitimu Makerere

BOB alimaliza kwa kufaulu vizuri masomo yake ya Uchumi Makerere na kisha akarejea Tanganyika.

9. BOB Aenda Masomoni LIVERPOOL, UK

Mwaka 1961, BOB alienda Chuo Kikuu cha Liverpool, UK ambako alisomea Sheria. Alifaulu vizuri masomo hayo vizuri ikiwa pia na mitihani ya mafunzo ya sheria (Middle temple), London.

10. BOB Arejea TZ

Mwaka 1965, BOB akarejea nchini na kuajiriwa kama Mwanasheria wa Serikali.

11. BOB Awa Meneja BOT

Mwaka 1968, BOB aliteuliwa kuwa Meneja BOT wa "Exchange Control" . Alihudumu nafasi hiyo hadi 1971. Wakati huo, Gavana alikuwa Mh. EDWIN MTEI ambaye alimpenda sana BOB kwa uchapakazi na Uzalendo wake, kama anavyotiririka:-

"Bob Makani alikuwa Mzalendo na mchapakazi hodari mimi nilipokuwa Gavana BOT. Mara kwa mara nilikuwa namsifia kwa Rais Nyerere. Hii ilipelekea Rais aninyang'anye hazina hiyo na kumteua kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu".

12. Rais NYERERE Amteua BOB kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu

Mwaka 1971, Rais NYERERE alimteua BOB kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

13. Rais NYERERE Amteua BOB Naibu Gavana BOT

Mwaka 1974, Rais NYERERE alimteua BOB kuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ambapo alikuwa chini ya Gavana CHARLES NYIRABU ambaye waliteuliwa pamoja mwaka huo.

14. BOB Ahudumu kwa utumishi Uliotukuka

BOB akiwa Naibu Gavana,  alishiriki kwa karibu sana kwenye maamuzi na mageuzi ya kiuchumi nchini, akifanya kazi hiyo kwa uaminifu na Uzalendo wa hali ya juu kwa Taifa lake.

15. BOB Awa Mjumbe Bodi Lukuki

Katika utumishi wake wa Umma, BOB alihudumu kwenye Bodi mbalimbali mf. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ndege, Mkurugenzi wa Bodi ya Williamson Diamonds, Mkurugenzi Bodi ya TZ Breweries, Mkurugenzi Bodi ya NBC nk.

16. BOB Awa Wakili wa Kujitegemea

BOB alihudumu kama Naibu Gavana kwa miaka 12 toka 1974 hadi 1986. Tarehe 4.4.1986, BOB aliapishwa kuwa Wakili wa kujitegemea na kupewa namba ya Uwakili 131 na mara moja akanzisha kampuni yake "Bob Makani & Co. Advocates".

17. BOB-: Mpenzi Kindakindaki wa LIVERPOOL FC

Kutokana na kusomea Sheria jijini Liverpool, BOB alilipenda sana Chama Kubwa Liverpool FC, na hilo lilikuwa wazi.

18. BOB Amfanya MZEE WA ATIKALI Kushabikia LIVERPOOL FC

MZEE WA ATIKALI alipata fursa kumtembelea Wakili BOB kwenye ofisi zake za uwakili zilizokuwa eneo la Co-cabs, Mnazi Mmoja, Dsm. BOB alimsimulia MZEE  WA ATIKALI jinsi alivyochezea Uganda Cranes na jinsi alivyoihusudu Liverpool FC na toka siku hiyo "MZEE WA ATIKALI  akawa shabiki mkubwa wa Liverpool FC ie MZEE WA ALLEZ ALLEZ ALLEZ LIVERPOOL FC!!!.

19. BOB Awa Mmoja wa Waasisi wa CHADEMA

Baada ya mfumo wa vyama vingi kuanzishwa nchini mwezi Julai 1992 kupitia Sheria ya Vyama vya Siasa, 1992,  BOB alikuwa ni mmoja wa Waasisi wa CHADEMA iliyosajiliwa Januari 1993 na kupewa Hati ya Usajili Na. 0000003. BOB kadi yake ya uanachama ilikuwa ni Na.3 akitanguliwa na Mh. EDWIN MTEI Kadi Na.1 na Mh. BROWN NGWILULUPI Kadi Na.2.

Waasisi wengine walikuwa VICTOR KIMESERA, PHILEMON NDESAMBURO, GEORGE WASIRRA, COSTA SHINYANGA, MARY KABIGI, EVARIST MAEMBE na MEDARD MUTUNGI.

20. BOB Amfanya MWALIMU Aisifu Katiba ya CHADEMA

BOB, akitumia weledi wake wa Sheria na uzoefu wake wa Uchumi, kwa kushirikiana na Waasisi wenzake, waliisuka vizuri sana Katiba ya CHADEMA. Mh. MTEI akampelekea Katiba hiyo Mwalimu  NYERERE huko Butiama. MWALIMU, bila kumung'unya maneno, aliisifu sana Katiba hiyo hadharani.

21. BOB Awa Katibu Mkuu wa Kwanza wa CHADEMA

BOB alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa CHADEMA na Mh. MTEI akawa Mwenyekiti. Viongozi hawa walifanya kazi kubwa sana "kukiuza" chama mikoani ambako walipata changamoto mf Morogoro walipigwa mawe, lakini hawakukata tamaa bali walikomaa hadi chama kikasimama.

22. BOB Awa Mwenyekiti CHADEMA

Mwezi Agosti 1998, BOB alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA na kuhudumu hadi Machi 2003. Baada ya hapo, BOB alibaki kuwa mshauri wa chama huku aliendelea na kazi zake za uwakili.

23. Afya ya BOB Yaanza Kutetereka

Mwaka 2009, BOB aliugua na mwaka uliofuata alipelekwa India  kwa  matibabu. Mwanzoni mwa mwaka 2012, BOB alipelekwa Nairobi, Kenya kwa matibabu pia.

24. BOB Aaaga Dunia

Majira ya saa 5 usiku, siku ya Jumamosi, tarehe 9.6.2012, BOB aliaga dunia akiwa njiani akikimbizwa Aga Khan hospitali. BOB aliagwa ukumbi wa Karimjee tarehe 11.6.2012 ambapo Rais KIKWETE aliongoza maelefu ya wakazi wa Jiji la Dsm kutoa heshma zao za mwisho. BOB alizikwa tarehe 12.6.2012  wilayani kwake Kishapu ambapo aliacha mke, watoto Dr. JULIE, GRACE, TUME, MOHAMED nk na wajukuu kadhaa.

25. TAMATI

Huyu ndiye marehemu BOB NYANGA MAKANI ambaye Bongolanders wengi walimtambua kwa umahiri wake kama Mwanasiasa tu. ATIKALI hii imetanabaisha bayana kuwa BOB alikuwa ni Kipanga aliyejaaliwa talanta lukuki ambazo alizitumia vizuri katika maisha yake. Kipaji chake cha hali ya juu cha kabumbu kilipelekea BOB aweze kuichezea Timu ya Taifa ya Uganda wakati yeye alikuwa Myanganyika! Hakuna raia mwingine yeyote wa Afrika Mashariki aliyeweza kufanya hivi hadi leo, ukimwondoa BOB.


KONGOLE KWAKO BOB NYANGA MAKANI!!!


BY MZEE WA ATIKALI ✍️✍️✍️



 

No comments: