Benki ya CBA (Commercial Bank of Africa (Tanzania) yatoa msaada wa Matanki ya Maji kwa Hospitali za Umma jijini Dar es salaam.

Benki ya Commercial Bank of Africa (CBA) Tanzania imetoa msaada wa matanki nane ya maji yasiyo na mkono kwa hospitali nne zilizochaguliwa jijini Dar es salaam kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka ya kusafisha mikono ambayo ni hatua muhimu katika kupambana na COVID-19.

Akikabidhi mchango huo Afisa Mtendaji Mkuu wa CBA, Gift Shoko amesema msaada huo ni sehemu ya hatua zilizochukuliwa na CBA kuunga mkono juhudi za serikali katika kupambana na kusambaa kwa COVID-19 nchini Tanzania.

"Commercial Bank of Africa (Tanzania) imejitolea kusaidia hospitali ziweze kutoa vifaa sahihi kwa watu wanaotembelea hospitali hizo ili kuwawezesha kutekeleza utaratibu wa kunawa mikono kwa sababu ni silaha muhimu ya kupambana na virusi vya corona. Mara baada ya kutambua kuwepo kwa ongezeko la mahitaji ya vifaa vya kunawia mikono, benki ya CBA ilianza kufanya mchakato wa kupata matanki kwaajili ya kuhifadhia maji katika kusaidia upatikanaji wa vifaa vya kunawia mikono katika hospitali ambako ndio sehemu muhimu kwaajili ya ustawi wa jamii ya Dar es salaam." Alifafanua bwana Shoko

"Kama tunavyofahamu, maambukizi ya virusi vya corona yanaweza kutokea kwa kugusa sehemu iliyoguswa na mtu mwenye virusi, hivyo tumehakikisha kwamba matanki ya maji yamewekewa kifaa cha kufungulia maji kwa kukanyaga kwa mguu ili kumlinda zaidi mtumiaji. 

Hospitali ambazo zimenufaika na msaada huo ni pamoja na Amana, Sinza, Mwananyamala na Lugalo. Hospitali hizi zinahudumia idadi kubwa ya watu kila siku, hivyo tuliamua kuanza na hizi. Ni matumaini yetu kwamba tutaweza kuzifikia hospitali nyingi zaidi katika siku zijazo" Alieleza zaidi bwana Shoko.

Ili kukuza ufahamu kuhusu Virusi vya Corona miongoni mwa wateja, benki ya CBA imeweka taarifa katika mfumo wa barua pepe, ujumbe mfupi wa maneno, mabango pamoja na kutumia mitandao ya kijamii (Facebook na Twitter) kutuma ujumbe wenye taarifa sahihi kwa umma kuhusu COVID-19 ni nini na ni jinsi gani ya kujilinda, Kujikinga na kuchukua hatua.

"Benki ya CBA imeweka kipaumbele kikubwa katika usalama wa wafanyakazi wake na wateja kwa kuweka dawa za kusafisha mikono (hand sanitizers) katika milango na katika vyumba ili ziweze kufikiwa na kutumiwa kwa urahisi na wafanyakazi wetu. Iwapo itatokea dharura benki ya CBA imeandaa vyumba maalumu kwaajili ya kushughulikia matukio ya dharura wakati msaada wa kitabibu unafuatiliwa, hii ni kwa Makao Makuu pamoja na katika matawi yetu yote nchi nzima" alihitimisha Shoko.

Vile vile benki ya CBA imeweka mfumo kwaajili ya idara ambazo sio lazima ziweko ofisini kuweza kufanya kazi nyumbani kwa kutumia vifaa vya kidigitali vya mawasiliano na uendelevu wa biashara kwa lengo la kupunguza safari na hatari ya kusambaa kwa COVID-19.



Mwakilishi kutoka kitengo cha Ugavi wa Hospitali ya Mwananyamala, Hiltruda Patrick (kushoto) akipokea matanki ya maji kutoka kwa Geofrey Kivamba wa Brandmiles kwa niaba ya Benki ya Commercial Bank of Africa (CBA) Tanzania ikiwa ni sehemu ya msaada wa matanki nane ya maji yasiyo na mkono kwa hospitali nne zilizochaguliwa jijini Dar es salaam ili kukabiliana na mahitaji yanayoongezeka ya kusafisha mikono ambayo ni hatua muhimu katika kupambana na COVID-19. Katikati ni Mfamasia wa hospitali hiyo, Simon Mbise.

No comments: