ZANZIBAR YARIPOTI WAGONJWA WATATU WAPYA WALIOAMBUKIZWA MARADHI YA CORONA (COVID-19).

Waziri wa Afya Hamad Rashid Muhamed

Na Ramadhani Ali – Maelezo 13.04.2020

Zanzibar imeripoti wagonjwa watatu wapya walioambukizwa maradhi ya Corona na kufanya jumla ya wagonjwa 12 walioambukizwa maradhi hayo hadi kufikia tarehe 13 Aprili 2020.

Akitoa taarifa kupitia Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Waziri wa Afya Hamad Rashid Muhamed amesema wagonjwa wote walioongezeka ni Watanzania na hawana historia ya ya kusafiri nje ya nchi katika siku za hivi karibuni.

Aliwataja wagonjwa hao kuwa ni wanaume wawili mmoja mkaazi wa Mwanakwerekwe na mwengine anatoka Bumbwisudi na mwanamke mwenye umri wa miaka 22 mkaazi wa Jang’ombe.

Hata hivyo alisema wagonjwa wawili waliokuwa wakipatiwa matibabu katika kituo cha Kidimni wameshapona na kuruhusiwa kurudi nyumbani huku wakitakiwa kuendelea kubaki ndani bila ya kuchanganyika na watu wengine kwa muda wa siku 14.

Alisema wagonjwa wengine wanaendelea kupatiwa matibabu katika kituo maalum cha Kidimni na kile cha Skukli ya JKU Mtoni kilichofunguliwa hivi karibuni kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa.

Waziri wa Afya alithibitisha kuwa wagonjwa wote waliopo katika vituo hivyo wanaendelea vizuri na afya zao zinaendelea kuimarika siku hadi siku.

Aliwataka wananchi kuchukua tahadhari za ziada na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Serikali na wataalamu wa Afya ili kuhakikisha wanazuia maambukizi mapya ya Corona.

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO

No comments: