USHAURI KWA WANAHABARI KUHUSU KUCHUKUA TAHADHARI ZAIDI KUJIKINGA NA MAAMBUKIZI YA CORONA
Siku ya Ijumaa Aprili 10, 2020 Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilitoa taarifa kwa umma juu ya mwenendo wa ugonjwa wa corona nchini. Katika taarifa hiyo Waziri wa afya alieleza idadi ya watu waliothibitishwa kupata maambukizi ya COVID-19 nchini kuwa ni 32. Kati ya hao, wagonjwa 24 wanaendelea na matibabu, watano wamepona na uwepo wa vifo vya wagonjwa watatu tangu ugonjwa huu ulipoingia nchini.
Tunatoa pole kwa ndugu, jamaa na familia za waliopoteza ndugu zao kutokana na ugonjwa huu unaosababishwa na virusi vya corona.
Wito wetu kwa Wanahabari na Wananchi
Kutokana na kuongezeka kwa visa vya corona nchini ambavyo inaonyesha vimeanza kusambaa ndani ya nchi (Local Transmission and not imported). Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa pamoja tunatoa ushauri kwa wanahabari, taasisi mbalimbali na wananchi kama ifuatavyo:
1. Kuchukua tahadhari zaidi na kutoa taarifa kwa wakati kwenye mamlaka husika endapo wakibaini mtu mwenye dalili za maambukizi ya virusi vya corona.
2. Tunawasisitiza waandishi wa habari, taasisi mbalimbali na wananchi kutumia teknolojia ya kisasa katika kufanya kazi zao au mikutano, kwa mfano kutumia Skype, Zoom, kupiga simu, WhatsApp N.K.
3. Tunashauri vituo vya habari nchini kupunguza vipindi vya kawaida na kuanza kutumia vipindi hivyo kutoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kujikinga na virusi vya corona. Wananchi wapewe nafasi ya kuuliza maswali na kujibiwa kutoka kwa wataalamu.
4. Waandishi wa habari wanapaswa kuzingatia kwa makini taratibu za kitaaluma, huku wakihakikisha kutumia vyanzo vya habari vya kuaminika kama vile Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani (WHO).
5. Wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari zaidi za kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona kwa kuzingatia Miongozo iliyotolewa na
MCT,(https://mct.or.tz/kipeperushi-corona/), THRDC (https://thrdc.or.tz/tamko-kuhusu-kukamatwa-kwa-waandishi-wa-habari-
arusha/), Shirika la Frontline Defenders https://www.frontlinedefenders.org/sw/statement-report/physical-emotional-and-digital-protection-while-using-home-office-times-covid-19 pamoja na elimu inayotolewa mara kwa mara na Wizara ya Afya https://moh.go.tz/en/covid-19-info.
6. Waandishi wa habari wanapaswa kuchunguza kwa makini aina ya matukio ambayo wanapanga kuhudhuria, kutokana na uwepo wa amri ya Serikali inayokataza mikusanyiko ya idadi fulani ya watu ili kujikinga na hatari ya kupata maambukizi ya virusi vya corona.
7. Wamiliki wa vyombo vya habari wanapaswa kuwawezesha waandishi wa habari usafiri binafsi au kutumia uber, gloves ukiwa, mavazi ya kujikinga kiafya kama vile suti ya kitabibu (bodysuit) na barakoa inayofunika uso gubigubi (full face mask).
8. Tunatoa ushauri kwa waandishi wa habari kufuata sheria na kuomba ruhusu kwa mamlaka husika endapo wanahitaji kukusanya taarifa kutoka maeneo ya karantini, hospitali na maeneo mengine yenye vizuizi vya kuingia.
9. Tunapenda pia kuishauri serikali kutenga maeneo maalumu ya watoa huduma kwa wagonjwa wa corona ili wasirudi majumbani mwao kuepusha maambukizi kwenye familia zao.
10. Tunatoa ushauri kwa watu wote mfano viongozi, Asasi za Kiraia, wanasiasa, viongozi wa dini, watu mashuhuli watumie vipaji vyao kuelimisha umma kuhusu namna ya kujikinga na virusi vya corona kwa kuzingatia maelekezo ya Wizara ya Afya.
11. Tunawahimiza waandishi wa habari pale wanapokusanya taarifa, kutumia maikrofoni ya kushikilia (directional mic) kwa kuishika kwa mbali iwezekanavyo, badala ya kutumia maikrofoni inayoshikizwa kwenye mavazi (clip mic).
12. Meza na vifaa vyote vya kufanyia uhariri, kompyuta, vichanganyio (mixers) na vifaa vingine vya kazi lazima vifutwe na vitakasa mikono kila baada ya kipindi au shughuli ya uhariri.
13. Ni muhimu kushirikisha Asasi za Kiraia, vyombo vya habari binafsi na vya serikali katika kamati zinazoundwa kukabiliana na virusi vya corona kwa kuwa AZAKi na vyombo vya habari ni wadau wakubwa katika kutatua changamoto za kijamii.
Kwa kutambua umuhimu wa kazi za waandishi wa habari, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania utatoa mafunzo kwa waandishi wa habari mikoa yote Tanzania bara na Zanzibar kwa njia ya mtandao ili kuwawezesha namna bora ya kufanya kazi za uandishi salama hasa katika kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya corona.
Imetolewa kwa pamoja na:
THRDC, MCT, TEF na UTPC
Dar es Salaam, Tanzania
Aprili 12, 2020.
No comments: