POLISI ECUADOR YAKUSANYA MIILI 800 MAJUMBANI

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

ECUADOR imesema kuwa polisi wameondoa karibu miili 800 katika wiki za hivi karibuni kutoka  majumbani huko Guayaquil ambako ni kitovu cha mlipuko wa virusi vya Corona (Covid -19) na hiyo ni baada ya ugonjwa huo kuzidi huduma za dharura, hospitali na huduma za mazishi, Shirika la utangazaji la Al-jazeera limeripoti.

Kiongozi wa timu iliyoundwa na serikali ya nchi ili kusaidia katika mapambano dhidi ya Covid -19  yenye polisi na wanajeshi, Jorge Wated amesema kuwa miili iliyokusanywa kutoka majumbani imezidi mia saba.

Mapema jumapili Wated kupitia ukurasa wake wa Twitter alichapisha taarifa iliyoeleza kuwa katika operesheni hiyo kwa wiki tatu zilizopita miili 771 ilikusanywa kutoka majumbani na miili 631 kutoka hospitali ambapo mochwari zilikuwa zimejaa.

Wated hakueleza kwa kina sababu zilizopelekea vifo hivyo na takribani miili 600 ilizikwa chini ya mamlaka nchini humo.

Ecuador imeripoti visa 7,500 vya Covid -19 tangu kiripotiwe kisa cha kwanza mapema Februari 29 huku ukanda wa Pwani wa Guayas ukiwa na maambukizi kwa asilimia 70 na visa 4,000 na hiyo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na serikali.

Majeshi na polisi walianza kuondoa miili kutoka majumbani wiki tatu zilizopita baada ya mifumo ya mochwari huko Guayaquil kupata hitilafu.

Katika mitandao mbalimbali ya kijamii kumekuwa na video zikionesha miili iliyopo barabarani pamoja na jumbe za kuomba msaada wa kuzikwa kwa ndugu zao na serikali ikachukua jukumu hilo.

Mapema Aprili Wated alieleza kuwa vifo vitikanavyo na Covid -19 kwa mwezi huu vinategemewa kufikia 2,500 hadi 3,500 katika eneo la Guayas. 

#Covid19 #CoronaVirus

No comments: