Mkurugenzi wa Kampuni ya Grative Tanzania Limited atakiwa kuripoti kituo cha Polisi

SERIKALI ya Wilaya ya Kaskazini “B” imemuagiza Mkurugenzi wa Kampuni ya Grative Tanzania Limited yenye Makao Makuu yake Dar es salaam kuripoti kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kaskazini “B” Asubuhi ya Ijumaa ya wiki hii kutoa maelezo ya kina kuhusiana na kuchelewa kumalizika kwa wakati Mradi wa Ujenzi wa Tangi la kuhifadhia Maji safi na salama linalojengwa katika Kijiji cha Kitope.

Agizo hilo limetanguliwa na lile alilopewa Mhandisi wa usimamizi wa Ujenzi huo aliyepo Zanzibar la kumtaka asitoke nje ya Zanzibar na kuripoti kwa Mkuu wa Polisi Wilaya kila siku saa 3.00 asubuhi kuanzia sasa hadi atakapojumuika na Mkurugenzi wake katika agizo hilo la siku ya Ijumaa.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Ndugu Rajab Ali Rajab kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kufuatia kuchelewa kukamilika kwa wakati mradi huo uliopangiwa kumalizika Mwezi Disemba Mwaka uliopita licha ya kuongezewa muda wa Miezi Mitatu iliyomalizika bila ya kufikia lengo.

“ Mhandisi wa Ujenzi ambae ndie msimamizi wa ujenzi wa Mradi huo lazima abakie Zanzibar wakati huu na kuripoti Polisi saa 3.00 asubuhi hadi amlete Mkurugenzi wake kwa ajili ya kulisawazisha suala hilo”. Alisisitiza Nd. Rajab.

Alitoa wito kwa Makampuni na Taasisi za Ujenzi kuhakikisha zinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Mikataba iliyowekwa iwe kwa Serikali na hata Taasisi Binafsi.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Kaskazini “B” alionya kwamba Serikali kamwe haitasita wakati wowote kuichukulia hatua Kampuni au Taasisi yoyote itakayokwenda kinyume na Mikataba yao vyenginevyo ni kuzorotesha Maendeleo na Ustawi wa Wananchi walio wengi.

Alisema ni vyema kwa wakati huu Uongozi wa Kampuni hiyo ya Grative Tanzania Limited ukajihakikishia unakamilika Mradi huo na kuukabidhi Serikalini si Zaidi ya Mwezi Juni Mwaka huu ili uondoe kero inayowakabili Wananchi wa eneo hilo ya upatikanaji wa huduma za Maji safi na salama.

Akitoa Taarifa ya kuzorota kwa ukamilikaji wa Ujenzi wa Mradi huo wa Tangi la kuhifadhia Maji safi na Salama hapo Kitope Mhandisi Msimamizi wa Mradi huo kutoka Kampuni ya Grative Tanzania Limited Nd. Goodluck Jackson Kyaro alisema uwasilishwaji mdogo wa fedha kutoka Uongozi wa juu wa Kampuni hiyo ndio unaochangia kudorora kwa mradi huo. 

Mhandisi Goodluck alisema mradi huo hivi sasa umesimama kwa vile hata fedha za kuwalipa wafanyakazi zimechelewa kuingizwa tokea Mwezi uliopita wa Machi Mwaka huu.

Mapema Mwakilishi wa Taasisi ya Tanzania Youth Icon inayosimamia Ujenzi huo kwa ufadhili wa Taasisi moja ya Umoja wa Mataifa Bwana Abdullah Ahmed Suleiman alisema Kampuni ya Ujenzi wa Mradi huo tayari imeshapatiwa fedha kwa Awamu Mbili sasa.

Bwana Abdullah alisema nusu ya gharama za Ujenzi huo takriban shilingi Milioni 41,147,000/- zimeshalipwa zikiwa ni sawa na asilimia 50% ya gharama za Ujenzi wote uliotegemewa kwa mujibu wa Mikataba iliyokubalika.

Mwakilishi huyo wa Tanzania Youth Icon alimueleza Mkuu huyo wa Wilaya kwamba Ujenzi huo licha ya kufikia hatua ya asilimia 40% lakini bado ipo hatua nyengine ya kukamilisha kufikia hadi usawa wa Tangi lenyewe.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
14/04/2020.
Muonekano wa Tangi la kuhifadhia Maji safi na Salama linalojengwa katika Kijiji cha Kitope ambalo limesita kukamilishwa na Mhandisi aliyepewa jukumu la ujenzi wake.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Rajab Ali Rajab akimuagiza Mkurugenzi wa Kampuni ya Grative Tanzania Limited kufika Ofisini kwa ODC wa Wilaya ya Kakasini B kutoa maelezo ya kuchelewesha Mradi wa Ujenzi wa Tangi la Kitope.
Mwakilishi wa Taasisi ya Tanzania Youth Icon, Abdulla Ahme Suleiman akitoa maelezo kwa Mkuu wa Wilaya jinsi Taasisi hiyo ilivyokuwa ikitoa fedha za ujenzi wa Maradi wa Tangi kwa Awamu Mbili sasa.
Mhandisi Msimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa Tangi la Kuhifadhia Maji safi kutoka Kampuni ya Grative Tanzania Limited Goodluck Jackson Kyaro akimpatia maelezo, Rajab yaliyopelekea kuchelewa kukamilika kwa madi wa Tangi hilo.
Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments: