MADAKTARI MUHIMBILI WATUMIA TEKNOLOJIA MPYA KUOKOA MAISHA YA WATOTO WANAOZALIWA UTUMBO UKIWA NJE

Na Leandra Gabriel, Michuzi TV

KWA mara ya kwanza madaktari bingwa wa upasuaji wa watoto kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili wamefanikiwa kuokoa maisha ya watoto wawili waliozaliwa wakiwa na tatizo la tumbo kuwa wazi na utumbo kuwa nje  (Gastroschisis) na kwa kutumia utaratibu madaktari hao wamefanikiwa kuwavalisha mifuko maalumu (Silo bags) ambayo haihusishi mtoto kufanyiwa upasuaji wala kupewa dawa za usingizi.

Akisoma taarifa hiyo leo jijini Dar es Salaam Daktari bingwa wa upasuaji wa watoto Dkt. Zaitun Mohamed Bokhary amesema kuwa awali kabla ya kuwepo kwa teknolojia hiyo uwezekano wa watoto wanaozaliwa tumbo wazi na utumbo nje kufariki dunia ilikuwa ni asilimia 100 lakini kwa teknolojia hii uwezekano wa kupona ni asilimia 100.

Amesema kuwa kabla ya teknolojia hiyo watoto wenye tatizo hilo ilibidi wafanyiwe upasuaji na kuvalishwa mifuko ya kawaida ambayo ufanisi wake ulikuwa mdogo na ulihusisha kupitia taratibu mbalimbali za upasuaji ikiwemo kupewa dawa za usingizi ambapo kutokana na uchanga wa watoto na muda ulikuwa unatumika kurejesha matumbo watoto walipata madhara mbalimbali ikiwemo vifo.

Dkt. Zaitun amesema kuwa kuanzia sasa mtoto akizaliwa na tatizo hilo atavalishwa mfuko maalumu unaotunza majimaji akiwa wodini ambapo kila siku watoa huduma na watakua wanausukuma utumbo kurudi tumboni kwa vipimo maalumu na katika kipindi cha siku tatu hadi tano utumbo huo utakuwa umerudi ndani kwenye hali ya kawaida na baadaye mtoto atafungwa tumbo kwa njia maalumu ambayo haiusishi kushonwa na nyuzi.

Vilevile amesema Kwamba katika kuhakikisha huduma hiyo inapatikana katika maeneo mengi nchini, tayari Hospitali ya Taifa Muhimbili imechukua jukumu la kutoa mafunzo maalumu kwa Hospitali zote za Kanda  zilizopo Mkoa wa Dar es salaam kuhusu namna ya kuwapa huduma ya kwanza watoto wanaozaliwa na  tatizo hilo kabla ya kuwapa rufaa ya kufika Muhimbili ambapo kwa sasa ndio sehemu pekee ambapo utaalamu huu unapatikana.

Pia amesema kuwa Hospitali hiyo itaendelea kutoa mafunzo hayo kwa hospitali nyingine nchini ili kuweza kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa na tatizo hilo.
 Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Zaituni Bokhary akimuhudumia mmoja wa watoto waliozaliwa wakiwa tumbo wazi na utumbo nje, ambaye kwa sasa amepona na anaendelea vizuri.

No comments: