KAWAMBWA AKABIDHI PIKIPIKI KWA MADEREVA BODA NA KUWAASA WAJASIRIAMALI KUUNDA VIKUNDI





*****************************
NA MWAMVUA MWINYI,BAGAMOYO
Mbunge wa jimbo la Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa amekabidhi pikipiki tatu kwa kikundi cha waendesha bodaboda kilichopo kitongoji cha Benki kata ya Dunda ,Huku akiwaasa wajasiriamali kutopuuzia kujiunga vikundi kwani vinasaidia kupata fursa mbalimbali kirahisi.
Pikipiki hizo ambazo zimenunuliwa kutokana na mkopo uliotolewa na halmashauri ya Bagamoyo kwa vijana, zimekabidhiwa kwa kikundi hicho kinachojulikana kwa jina la Umoja wa Madereva wa Bodaboda Stendi Geti namba 4, (UMABOS G4).
Akizungumza wakati wa kukabidhi pikipiki hizo, Mbunge huyo wa jimbo la Bagamoyo Dkt. Shukuru Kawambwa aliwapongeza vijana hao kwa kuchangamkia fursa na kwamba wao ni mfano wa kuigwa.
Alisema Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wake Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Magufuli inawajali wananchi wa hali ya chini ndiomana kila halmashauri kuna mfuko kwaajili ya vijana, kinamama na walemavu ambapo makundi hayo hukopeshwa na kurejesha bila ya riba.
Alisema serikali haiwezi kumpa fedha mtu mmoja mmoja lakini inatoa kwa vikundi ili iwe rahisi kuwahudumia watu wengi wenye uhitaji kwa wakati mmoja. 

Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Dunda, Dickson Makamba aliwapongeza vijana hao na kusema kuwa hao ni vijana wa mfano katika kata yake. 

Alisema kikundi hicho hakina muda mrefu toka kuanzishwa kwake lakini mafanikio yake ni makubwa katika kipindi kifupi ukilinganisha na vikundi vingine ambavyo vina muda mrefu. 

Awali akisoma taarifa ya kikundi Katibu wa kikundi hicho Abdalla Shabani Jongo alisema malengo yao ni kupata pikipiki tano na kwamba mpaka sasa wamefanikiwa kupata pikipiki tatu .

No comments: