Kamati kitaifa ya Makatibu Wakuu 14 ya kukabiliana na virusi vya Corona nchini imetembelea Hosteli za Magufuli katika Chuo Kikukuu cha Dar es salaam jijini humo ambako wasafiri kutoka nchi za nje wamepelekwa karantini kwa siku 14, huku wasafiri 72 wakiruhusiwa kurejea nyumbani baada ya vipimo kuonyesha hawana maambukizi ya Covid-19.
Wasafiri 226 kutoka nchi mbalimbali za nje walipelekwa karantini katika hosteli hizo na kwamba wasafiri wasafiri 72 wameruhusiwa kurejea nyumbani na hivyo wamebaki wasafiri 154.
Hayo yameelezwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt.Rashid Mfaume wakati akitoa taarifa kwa Kamati hiyo ya kukabiliana na virusi vya Corona ambayo imetembelea Hosteli za Magufuli, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani na kituo cha Kisoka ambacho kipo kilometa moja kutoka Hospitali ya Muhimbili-Mloganzila.
Akizungumza katika ziara hiyo, Katibu wa Makatibu wakuu, Dkt. Zainab Chaula ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amesema Kamati hiyo imetembelea maeneo hayo ili kupata taarifa za Maendeleona mafanikio ya huduma za afya za kukabiliana na maambukizi ya Covid-19 ambazo zinatolewa na wataalamu wa afya.
Dkt. Chaula amesema katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, jengo la kulaza wagonjwa wa Covid-19 limekamilika na kwamba wataalamu wako tayari kupokea wagonjwa wakati wowote kuanzia sasa.
“Kituo hiki au jengo hili ambalo lina vitanda 40, hivi sasa hakijapokea wagonjwa lakini wakipatikana tutawaleta hapa kwa ajili ya kuwahudumia. Pia nawashukuru Makatibu wakuu wenzangu kwa kushiriki kutembelea vituo hivi ambavyo vimeandaliwa na Serikali kwa ajili ya kukabiliana na maambukizi ya Covid-19,” amesema Dkt. Chaula.
Katika hatua nyingine, Serikali inajenga kituo cha kisasa cha magonjwa ya mlipuko kitakacho gharimu shilingi bilioni 7 na itakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 200 ambacho kipo eneo la Kisoka, kilometa moja kutoka Hospitali ya Mloganzila jijini Dar es Salaam.
Meneja Mradi wa Ujenzi wa kituo hicho Kanali Solomoni Shausi amesema kwamba mradi huo unajengwa na Suma JKT na kwamba baadhi ya majengo yatakamilika Aprili 30, mwaka huu.
|
No comments: