Dkt.Kijazi:Ongezeko la joto duniani,limesababisha mabadiliko ya hali ya hewa

Na Karama Kenyunko-Michuzi TV

KILA ifikapo Machi 23 kila mwaka,dunia mzima huadhimisha siku ya hali ya hewa duniani. Ni siku ambayo Mkataba wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ulisainiwa mwaka 1950. Kwa kawaida siku hii huadhimishwa na kila nchi mwanachama wa shirika hilo. 
 
Taasisi za Hali ya Hewa, zikiwa ni Mamlaka zilizopewa jukumu la kutoa na kusimamia huduma za hali ya hewa katika nchi wanachama wa WMO,hutumia siku hii kuonesha na kueleza huduma wanazotoa katika kuhakikisha usalama wa watu na mali zao dhidi ya athari zitokanazo na hali mbaya ya hewa. Kwa hapa nchini, shughuli zote zinazohusiana na masuala ya hali ya hewa husimamiwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
 
 TMA ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 2019 kwa mujibu wa sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. TMA iko chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sekta ya uchukuzi na imepewa jukumu la kutoa na kudhibiti huduma za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo, TMA ikiwa miongoni mwa Taasisi 192 za nchi wanachama wa WMO inaungana na Jumuiya ya hali ya hewa duniani kote kusherehekea Siku ya Hali ya Hewa duniani (WMD). 
 
Katika kusisitiza na kuhamasisha umuhimu wa huduma za hali ya hewa katika mipango na maamuzi kwenye sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii, sherehe za WMD zimekuwa zikiadhimishwa kwa kaulimbiu maalumu. Ambapo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi amesema kaulimbiu ya mwaka huu ni “Hali ya Hewa na Maji (Climate and Water)”, ambapo kauli hiyo inaenda sambamba na kaulimbiu ya Siku ya Maji Duniani kwa mwaka 2020, ambayo imejikita katika athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwenye sekta ya maji. 
 
Dkt.Kijazi ambae pia ni Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), amesema hewa na Maji inafafanua uhusiano uliopo kati ya hali ya hewa na rasilimali maji, pamoja na umuhimu wa kutumia huduma za hali ya hewa katika maendeleo ya sekta ya maji.
 
 Aidha,Dkt.Kijazi amesema kupitia siku hii ni vyema awafahamishe wadau wa huduma za hali ya hewa hapa nchini kwamba kwa mujibu wa taratibu za mgawanyo wa majukumu katika Umoja wa Mataifa,Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) limepewa jukumu la kusimamia masuala ya hali ya hewa na maji. 
 
Amesema Taasisi za Hali ya Hewa na Maji (NMHSs) katika nchi wanachama wa WMO hufanya uangazi wa hali ya hewa na maji na data za hali ya hewa na maji hutumika katika kutoa taarifa za mwelekeo wa hali ya hewa na maji ili kusaidia maamuzi katika vikao vya Umoja wa Mataifa vinavyohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi. 
 
Mkurugenzi huyo anasema ongezeko la joto duniani (global warming) linasababisha changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na limeathiri kwa kiasi kikubwa mifumo ya mzunguko wa maji kutokana na kubadilika kwa mifumo ya mikondobahari, mvukizo wa anga, ufanyikaji wa mawingu na mtiririko wa maji kwenye uso wa dunia. "Athari hizo zinatokana na uhusiano uliopo wa moja kwa moja wa mifumo ya hali ya hewa na mzunguko wa maji.
 
Changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa imeathiri pia upatikanaji na ubora wa maji na kusababisha upungufu wa maji yanayohitajika kwa matumizi mbalimbali,"amesema Dkt.Kijazi Amesema mabadiliko ya hali ya hewa yanasababisha mabadiliko ya mfumo wa mzunguko wa maji kwa namna tofauti tofauti, mfano, maeneo yenye joto zaidi hupata mvukizo zaidi wa maji kutoka baharini, ziwani, ardhini na kwenye mimea.
 
 "Anga ililopo katika eneo lenye joto zaidi lina uwezo wa kuhifadhi unyevunyevu kwa asilimia nne zaidi kwa kila ongezeko la nyuzi joto moja katika kipimo cha Celcius, na kusababisha kufanyika kwa mawingu ng’amba ambayo huambatana na mvua kubwa na ngurumo",anasema Dkt. Kijazi Mkurugenzi huyo amesema kuongezeka kwa joto husababisha mvukizo wa maji kutoka udongoni na kufanya ardhi kuwa kame zaidi na udongo kuwa mgumu, hali hiyo husababisha maji kushindwa kuingia udongoni pindi mvua inaponyesha, badala yake maji hutiririka kukimbilia kuelekea mitoni, ziwani au baharini, na kuiacha ardhi kuendelea kuwa kame. 
 
Amesema matokeo yake ni uwezekano wa kuongezeka kwa matukio ya ukame na upungufu wa maji safi na salama. Aidha,ongezeko la joto katika maji ya mito,maziwa, bahari na mabonde ya maji husababisha uhaba wa hewa safi ya oksijeni katika maji na kupelekea vifo kwa viumbe hai wanaoishi kwenye maji.
 
 "Matukio ya mvua kubwa na ongezeko la mtiririko wa maji pia husababisha usafirishwaji wa udongo, vijidudu vya magonjwa na kemikali kama vile mabaki ya mbolea na pembejeo kutoka maeneo mbalimbali yakiwemo mashamba, viwanda na mashimo ya maji taka kuelekea kwenye vyanzo vya maji,"amesema Aidha, miongoni mwa athari za mabadiliko ya hali ya hewa, Dkt. Kijazi amesema ni ongezeko la kina cha bahari duniani kote, husababishwa na mambo makubwa mawili,kutanuka kwa maji ya bahari kutokana na kuongezeka kwa joto la maji na pili ni kuyeyuka kwa barafu katika maeneo yenye barafu, hususan katika uzio wa actic na antaktika. 
 
Amesema ongezeko hilo la kina cha bahari linahatarisha miundombinu, mazingira na maisha ya jamii zinazoishi maeneo ya fukwe za bahari na visiwa, na kuathiri ubora wa maji kwa kusababisha mwingiliano wa majichumvi na vyanzo vya maji baridi hali inayopelekea hitaji la kutumia teknolojia yenye gharama kubwa kusafisha maji hayo. 
 
Kutokana na shughuli mbalimbali zinazotegemea maji kwa namna moja au nyingine, Dkt. Kijazi amesema mabadiliko hayo katika mifumo ya maji yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa yanaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa maisha ya viumbe katika uso wa dunia katika siku za usoni. "Hali hii inaonesha kwamba hali ya hewa ina mchango mkubwa na wa pekee katika mtawanyiko na upatikanaji wa maji katika uso wa dunia, pamoja na ubora wa maji yanayohitajika kwa shughuli za kiuchumi na kijamii kwa maendeleo endelevu,"amesema .
 
Amesema kwa msimu wa mvua za Oktoba hadi Desemba (vuli), 2019 kulikuwa na mvua nyingi zaidi katika mwezi Oktoba na Desemba. Aidha, katika mwaka 2020 matukio ya mafuriko yametokea katika maeneo mbalimbali ya nchi hususan mkoani Lindi. "Inatazamiwa kuwa, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, matukio ya mafuriko na ukame yataongezeka kwa wingi na ukubwa na hivyo kusababisha athari katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo sekta ya maji, nishati, usafirishaji na kilimo,"amesema. 
 
Dkt.Kijazi amesema pamoja na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, na athari zake katika mfumo wa mzunguko na upatikanaji wa maji, taarifa za hali ya hewa za sehemu husika zitasaidia katika kupanga shughuli za kiuchumi na kijamii zinazotegemea upatikanaji wa maji. Mkurugenzi huyo amesema taarifa hizo ni pamoja na data za hali ya hewa za kipindi kirefu ,utabiri wa hali ya hewa na matazamio ya mabadiliko ya hali ya hewa. 
 
Hivyo, ni muhimu kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu hali ya hewa ya eneo husika na kutumia taarifa za hali ya hewa. Mkurugenzi huyo amesema katika ngazi ya kidunia, Programu ya Kidunia ya Huduma za Hali ya Hewa inayoongozwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani “Global Framework for Climate Services (GFCS)” ndiyo programu inayoongoza jitihada za matumizi ya huduma za hali ya hewa katika mipango ya maendeleo. 
 
Katika kutekeleza programu hiyo kwenye ngazi ya kitaifa kwa nchi wanachama wa WMO, Dkt. Kijazi amesema TMA inatekeleza Programu ya Kitaifa ya Huduma za Hali ya Hewa “The National Framework 6 for Climate Services (NFCS)”, ambayo ina malengo ya kuboresha huduma za hali ya hewa katika sekta zilizoathiriwa zaidi na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo sekta ya maji. Amesema katika kutimiza mahitaji ya wadau na matakwa ya programu ya NFCS pamoja na sheria iliyoanzisha TMA, mamlaka hiyo hufanya shughuli za uangazi wa masuala ya hali ya hewa. 
 
Amesema TMA hufanya uangazi kupitia mtandao wake wa vituo vya hali ya hewa vilivyopo nchi nzima, ambavyo vinajumuisha vituo vilivyopo kwenye uso wa dunia nchi kavu, vilivyopo bandarini na vilivyopo katika anga la juu ambavyo vinajumuisha mtando wa RADAR (upper air stations). Aidha, Dkt. Kijazi amesema TMA hutoa utabiri wa hali ya hewa unaotumika katika mipango kwaajili ya shughuli za kijamii na kiuchumi, utabiri unaotolewa na TMA ni pamoja na utabiri wa kila siku (saa 24), siku tano, siku kumi (dekadal forecast), mwezi, msimu na tahadhari za hali mbaya ya hewa (severe weather warnings and alerts).
 
 "Tabiri hizi za hali ya hewa ni kwa jamii yote kwa ujumla, zikiwa na ushauri unaolenga sekta ambazo shughuli zake hutegemea zaidi hali ya hewa na maji. Hutoa taarifa mahsusi kwa sekta mahsusi kama vile sekta ya usafiri wa anga na usafiri wa kwenye maji,"amesema. Utabiri huo husambazwa kwa njia mbalimbali zikiwemo tovuti ya TMA (www.meteo.go.tz), radio, runinga, mitandao ya kijamii (facebook, twitter, Youtube, na WhatsApp), magazeti na mfumo wa kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa njia ya simu za mkononi (FarmSMS). TMA imeendelea kupata mafanikio zaidi katika kutekeleza mpango mkakati wake. 
 
Aidha, Dkt. Kijazi amesema TMA imefanikiwa kuzindua jarida la huduma za hali ya hewa, ambalo ni mahsusi kwa kuwafikia wadau na jamii yote kwa ujumla ikiwemo sekta ya maji. Katika eneo la vifaa vya hali ya hewa, TMA imeendelea na mkakati wake wa kuboresha vifaa kwa kununua vifaa vya kisasa na kuondoa vifaa vinavyotumia zebaki. Amesema katika kuhakikisha TMA inaboresha huduma zake na kuchangia katika jitihada za kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, TMA imeendelea kufanya tafiti mbalimbali zinazohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa ambazo zimechapishwa katika machapisho mbalimbali ya kisayansi ya kimataifa. 
 
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe katika taarifa yake amesema kwa upande wa Tanzania, TMa ina jukumu la kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa utabiri wake ambao huchangia kulinda vyanzo vya maji na hivyo kuboresha upatikanaji wa rasilimali maji. Amesema upatikanaji wa rasilimali maji ni muhimu katika kuchangia maendeleo ya Taifa na malengo ya Umoja wa Mataifa ya maendeleo endelevu. 
 
Huduma za hali ya hewa ni muhimu katika malengo hayo hususani lengo namba saba la SDG7 ambalo linahusiana na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi. "Tanzania inaendelea kutekeleza maridhiano ya kimataifa katika sekta ya hali ya hewa kwa kuhakikisha Mamlaka ya Hali ya Hewa inatoa huduma za hali ya hewa katika viwango vinavyokubalika kimataifa,"amesema Mhandisi Kamwelwe. 
 
Mhandisi Kamwelwe amesema utekelezaji huo ni pamoja na kuijengea uwezo Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa upande wa vifaa na wataalamu ili kuhakikisha wanafuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazohitajika nchini, kikanda na kimataifa kwa matumizi ya sekta zote ikiwa ni pamoja na sekta ya maji. Amesema, 2019 Serikali ilipitisha sheria ya kuhuisha Wakala wa Hali ya Hewa nchini kuwa Mamlaka kwa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa namba mbili ya 2019. 
 
Sheria hiyo inaiwezesha mamlaka kutekeleza majukumu yake kitaifa, kikanda na kimataifa na kutoa huduma za hali ya hewa kwa jamii. Pia, amesema sheria iliyounda Mamlaka hiyo inaipa nguvu za kisheria za kudhibiti huduma za hali ya hewa hapa nchini na kukusanya mapato yanayotokana na matumizi ya huduma za hali ya hewa zinazotumiwa kibiashara. Aidha, amesema Sheria hiyo inaitambua Serikali kama mdau mkubwa wa huduma zinazotolewa kwa matumizi ya wananchi (Public Good) hususan tahadhari za hali mbaya ya hewa. 
 
"TMA inatarajiwa kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa nchini, hivyo sheria hii imehakikisha uwakilishi,ushirikishwaji, mabadiliko ya kimtazamo na uwajibikaji wa wadau wote ikiwa ni pamoja na sekta binafsi na jumuiya za kijamii,"amesema Mdandisi Kamwelwe.
 
 Katika kuhakikisha kuwa TMA inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi ili kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii hapa nchini, Kamwekwe amesema Serikali inaendelea kuijengea uwezo mamlaka hiyo ili iweze kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kuboresha utabiri wa hali ya hewa. 
 
"Taarifa za hali ya hewa ni za muhimu sana katika kutoa maamuzi na kuweka mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, taarifa na huduma za hali ya hewa husaidia na kuongeza uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na vilevile kuchangia katika maendeleo endelevu,"amesema Waziri huyo amesema huduma za hali ya hewa zitolewazo husaidia watumiaji wa huduma hizo kupanga vyema shughuli zao ambazo ni pamoja na mipango ya utoaji wa huduma za maji mijini, kilimo, mifugo, maendeleo ya uvuvi, uzalishaji wa nishati na uratibu wa maafa miongoni mwa sekta nyingine. 
 
Aidha, katika jitihada za kuboresha huduma za hali ya hewa nchini, Serikali imeendelea kuongeza uwezo wa TMA kwa kuboresha mtandao wa Taifa wa vituo vya upimaji wa hali ya hewa ili kuboresha upatikanaji wa data na usahihi wa utabiri wa hali ya hewa. Amesema Serikali inaendelea kuongeza uwezo wa TMA kufuatilia na kupima hali ya hewa na kuboresha utabiri wa hali ya hewa kwa matumizi katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii pamoja na kufanya maamuzi ya mipango ya maendeleo katika sekta hizo. 
 
"Kwa kuzingatia hatua kubwa ya maendeleo iliyopigwa katika nyanja ya teknolojia na mahitaji yake katika sayansi ya hali ya hewa, Serikali inaipongeza TMA kwa kuendeleza ubunifu na matumizi ya teknolojia katika kuboresha huduma wanazotoa hapa nchini' "Kwa kutambua juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais, Dkt. John Magufuli ambapo imeboresha utendaji wa TMA katika utoaji wa huduma bora za hali ya hewa, hatuna budi kutumia huduma hizi ili kuboresha shughuli zetu za kila siku na vilevile kufanya kazi kwa pamoja ili kuendelea kuboresha huduma hizi kwa siku zijazo,"amesema.
 
 Amesema uwekezaji wa Serikali katika utoaji wa huduma za hali ya hewa hususani katika kuboresha miundombinu ni pamoja na ununuzi wa Rada 4 za hali ya hewa kwa lengo hilo hilo la kuboresha upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa nchini. 
 
Amesema Rada hizo zimefungwa Mwanza na Dar es Salaam na zingine tatu ziko katika hatua ya ununuzi ambazo zitafungwa Mtwara, Mbeya na Kigoma, ili kukamilisha mtandao wa Rada zitahitajika Rada zingine mbili ambazo zitafungwa Dodoma na Kilimanjaro. Pia, amesema kwa kutambua ongezeko la uhitaji wa huduma za hali ya hewa na changamoto zinazotukabili ambazo zinahitaji kutatuliwa, Serikali itaendelea kuwekeza ili kuendelea kuboresha huduma za hali ya hewa na maji kwa kuongeza uwezo wa wataalamu na miundombinu. 
 
"Kwa kuzingatia maboresho yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika katika utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini, ni vyema kuongeza juhudi katika kutumia huduma hizi katika mipango ya sekta zote za kiuchumi na kijamii na utekelezaji wa miradi ya kitaifa kama vile ujenzi wa miundombinu, uendelezaji na uzalishaji wa nishati inayotokana na maji, kilimo na rasilimali maji,"amesema.
 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam kuelezea tathmini ya hali ya Hewa kwa mwaka 2019. Pichani chini Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi akiwa katika mkutano huo.

No comments: