DC WA SINGIDA AJA NA OPERESHENI TOKOMEZA CORONA

Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili akiwa ndani ya basi la Kampuni ya Kiazi Kitamu akiwaeleza abiria mbinu za kujikinga na Virusi vya Corona (COVID-19) alipokuwa kwenye Operesheni maalum ya Tokomeza Corona Katika Manispaa ya Singida kwenye Kituo Kikuu cha mabasi. (Picha na. Peter Kashindye).
1 Madereva na Mawakala wa mabasi kwenye Kituo Kikuu cha mabasi ya Mkoa wa Singida (Misuna) wakionyesha jinsi ya kutumia vitakasa mikono ili kukabiliana na ugonjwa wa Corona (COVID-19) kwa Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili (Hayupo pichani) alipofanya Operesheni Maalum ya Tokomeza Corona Katika Manispaa ya Singida kuona utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya kujikinga na ugonjwa huo (Picha na. Peter Kashindye).
Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili (aliyenyanyua mkono) akihoji uelewa wa kujikinga na virusi vya Corona (Covid-19) mahali pa kazi kwenye maduka ya kuuzia nyama alipofanya Operesheni Maalum ya Tokomeza Corona Katika Manispaa ya Singida kwenye Soko Kuu la Singida Mjini. (Picha na. Peter Kashindye).
Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili akiwasisitiza wafanyabiashara wadogo juu ya matumizi sahihi ya vitakasa mikono alipofanya Operesheni maalum ya Tokomeza Corona Katika Manispaa ya Singida kwenye Soko Kuu la Singida Mjini. (Picha na. Peter Kashindye).
Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskasi Muragili (aliyenyanyua mkono) akitoa maelekezo kwa madereva na mawakala kuzingatia miongozo iliyotolewa na Wizara ya Afya juu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona (Covid-19). (Picha na. Peter Kashindye).
Na John Mapepele ,Singida

Mkuu wa Wilaya ya Singida Injinia Paskasi Damian Muragili amefanya Operesheni Maalum kwenye maeneo mbalimbali ya Mji wa Singida kutoa elimu na kuona jinsi wananchi walivyotekeleza maelekezo ya Serikali kuhusu ya kujikinga na ugonjwa unaoambukizwa na Virusi vya Corona (Covid 19).

Licha ya kutoa elimu hiyo pia amewapiga faini za hapo hapo watu waliobainika kukiuka maagizo huku akisisitiza kuwa Serikali itawanyang’anya lesseni za biashara na kufunga biashara hizo wote ambao wataendelea kukaidi maelekezo hayo

Mhandisi Muragili amefanya Operesheni hiyo maalum akiwa na Kikosi Kazi cha wataalam mbalimbali kwenye Wilaya yake ambapo ilianza alfaji hadi usiku wa kuamkia leo ambapo alitembelea maeneo yote ya huduma katika Mji wa Singida iliyojumuisha maeneo ya Standi Kuu ya Mkoa wa Singida ya Misuna, Soko Kuu la Singida na maeneo ya biashara ya Bajaji.

Akiwa katika Soko Kuu la Singida, Mkuu wa Wilaya alifanikiwa kukuta maduka ya nguo ya Kikundi cha Ushonaji cha Singida yakiwa hayana vitakasa mikono lakini wauzaji walikuwa wakiendelea na shughuli za biashara na kuwatoza faini ya shilingi elfu 50 papo hapo.

Akilipa faini hiyo baada ya kukiri kosa hilo, Mwenyekiti wa kikundi hicho ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Soko Kuu Singida Amina Msaghaa aliomba samahani kwa Mkuu wa Wilaya na kuahidi kutoendelea kufanya kosa hilo na kwamba faini hiyo imekuwa fundisho kwao na kwa hiyo wao kama kikundi watakuwa mfano wa kuwafundisha wafanyabiashara wengini

“Mhe. Mkuu wa Wilaya naomba kukueleza kuwa tumetoa faini hii kwa masikitiko makubwa, lakini hii inatupa ujasiri wa kushirikiana na Serikali yetu kuhamasisha kuhusu kujikinga na ugonjwa huu, naahidi tutakuwa walimu wazuri” alisitiza Msaghaa

Mwenyekiti wa Waendesha Bajaji Mkoa wa Singida Hemed Juma amesema katika kupambana na ugonjwa wa Corona chama chao kimechukua tahadhari zote zinazoelekezwa na Serikali kuhusu ugonjwa huu na kwamba yoyote atakayekaidi atashughulikiwa kikamilifu na chama chao ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwenye Vyombo vya Sheria.

Akifanya ukaguzi kwenye mabasi yanayoingia na kutoka kwenye Stendi Kuu Mkuu wa Wilaya amesema abiria wanatakiwa kutumia vitakasa mikono wanapoingia na kutoka kwenye mabasi hayo kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huu

Aidha amesema Operesheni hiyo imeanza na itakuwa endelevu na ya kushitukiza kila wakati hadi ugonjwa huu utakapoisha.

Amewataka kila mwananchi wa Wilaya ya Singida kuwa mzalendo kwa kuzingingatia maelekezo ya Wizara ya Afya ya kujikinga na ugonjwa huu kwa kujitenga na kuchukua hatua zinazotakiwa ili kujilinda na kuwalinda wengine na kwamba wanapohisi kuwa kuna mgeni ambaye ameingia na hajapimwa watoe taarifa kwenye Mamlaka zilizo katika maeneo yao

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi katika siku za hivi karibuni ameanza ziara maalum ya kuhamasisha wananchi wa mkoa wake kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huu kwa kufuata taratibu zote zinazotolewa na wataalam wa afya za kudhibiti na kujikinga na ugonjwa, wa Covid-19, kumwomba Mungu na kuendelea kuchapa kazi ili kunusuru kupoteza maisha na kushuka kwa uchumi wa nchi yao

Akiwa kwenye Soko maarufu la viazi lishe kwenye Kitongoji cha Kideka katika Kijiji cha Nkunikana aliwapongeza wafanyabiashara hao kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 kwa kuandaa miundombinu ya maji ili kunawa mikono kwa sabuni katika maji yanayotiririka wakati wote.

Aidha aliwataka wakulima wa viazi lishe kuendelea kulima kwa bidii ili wananchi wapate lishe bora kutokana na viazi hivyo na majani yake ambapo alisisitiza kuwa katika kipindi hiki ni muhimu kusanitaizi mikono na kusanitaizi afya zao

“Naelekeza wakulima waache visingizio nao waendelee kwenda mashambani kujitenga na kulima kwa bidii katika kipindi hiki ili waweze kupata mazao mengi na wakati huo huo watekeleze matakwa ya Serikali ya kujitenga na mikusanyiko isiyo ya lazima ambayo ingeweza kusababishia maambukizi endapo mmoja ana maambukizi.”

No comments: