Bilioni 16 Zaleta Mageuzi Miundombu ya Barabara Manispaa ya Singida

Muonekano wa taa katika barabara yakuingia mjini Singida kama ilivyokutwa Machi 27, 2020 baada ya kutekelezwa kwa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mji huo.
Moja ya barabara za Halmashauri ya Manispaa ya Singida kama inavyoonekana baada ya ujenzi na uwekaji wa taa kukamilka.
Muonekano wa Stendi Kuu ya Halmashauri ya Manispaa ya Singida inayohdumia mabasi ya ndani na nje ya nchi kama inavyoonekana katika picha, mradi huo umetekelezwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 3 na kuwezesha mapato kuongezeka kutoka shilingi laki 300,000/- hadi Shilingi milioni 1.5 kwa siku kwa sasa.

(Picha zote na Aboubakari Kafumba- MAELEZO Singida)

*******************************

Frank Mvungi- MAELEZO

Shilingi bilioni 16 zimetumika kujenga barabara za lami katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida ikiwa ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano kujenga miundombinu ya kisasa.

Akizungumza katika mahojiano maalum mjini Singida, Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) katika Manispaa hiyo Mhandisi Lambert Bayonaamesema ujenzi huo umetatua changamoto ya ubovu wa barabara katika manispaa hiyo na kuifanya kuwa moja ya maeneo ya kuvutia kwa kuwa na miundombinu yakisasa ikiwemo taa za barabarani.

“Barabara zenye urefu wa kilomita 9.85 zimejengwa kwa kiwango cha lami zikiwa na njia za waenda kwa miguu, mitaro ya kutiririsha maji, sambamba na kujengwa kwastendi ya kisasa ya Misuma iliyogharimu Shilingi bilioni 3 ikiwa na uwezo wa kuhudumia mabasi makubwa zaidi ya 72 kwa wakati mmoja, kuegesha bajaji na bodaboda na maeneo ya kufanyia biashara”, alisisitiza Bayona.

Akifafanua, amesema kuwa ujenzi wa stendi hiyo umewezesha mapato ya Halmashauri kuongezeka kutoka shilingi laki tatu zilizokuwa zikikusanywa awali kabla ya ujenzi huo hadi shilingi milioni 1.5 kwa sasa baada ya ujenzi huo.

Kujengwa kwa stendi hiyo kumeenda sambamba na ujenzi wa stendi ndogo ya daladala inayochangia katika kurahisisha usafirishaji katika Manispaa hiyo.

Akizungumzia faida za kujengwa miundombinu hiyo, Bw. Bayona amesema kuwa imechochea ukuaji wa uchumi kwa wananchi, kupunguza gharama za usafiri, kuboresha mazingira na kufanya mji huo kuwa wa kisasa ,kupungua kwa ajali, muda wa kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine umepungua na kuongezeka kwa mapato ya halmashauri.

Aidha, awamu ya pili ya ujenzi wa barabara za Manispaa hiyo itahusisha kilomita takribani 10 na usanifu wa mradi huo tayari umekamilika.

Kwa upande wake mmoja wa wakazi wa Manispaa hiyo, Bi. Maimuna Hamis amesema kujengwa kwa stendi hiyo na barabara hizo kumewawezesha wananchi kufanya shughuli za kiuchumi na kuongeza tija katika uzalishaji.

“Naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutujengea barabara za kisasa zenye taa na stendi nzuri hapa Singida”, alisisitiza Bi Maimuna.

Naye Meneja wa Stendi hiyo, Bw. Gaudensi Kaziyoba amesema kuwa ujenzi wa stendi umetatua changamoto ya wasafiri kukaa katika maeneo yasiyo na ubora wanaposubiri mabasi kuelekea maeneo mbalimbali mkoani humo, nje ya mkoa huo na nchi jirani.

Aliongeza kuwa usalama wa abiria na mali zao umeimarishwa katika eneo lote la stendi hali inayowezesha wananchi kufurahia ujenzi wake.

Ujenzi wa miundombinu ya barabara, stendi na mingine katika sekta za elimu, afya, maji, nishati na nyingine kunatajwa kuwa kichocheo cha maendeleo katika Mkoa waSingida na Halmashauri zake zote.

No comments: