VIJIJI VINAVYOZUNGUKA MRADI URAMBO VIPATIWE UMEME NDANI YA MIEZI SITA-DKT.KALEMANI
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akikata utepe kuashiria uwashaji umeme katika Kijiji cha Mabundulu wilayani Urambo, Mkoa wa Tabora. Wa Pili kushoto ni Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa tatu kushoto), akitoa maelekezo wa wataalam wa TANESCO wanaosimamia ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Urambo ambacho kinajengwa chini ya mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Tabora hadi Kigoma.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Mabundulu wilayani Urambo, Mkoa wa Tabora wakati alipofika kijijini hapo kuwasha umeme. Wengine ni viongozi mbalimbali kutoka wilayani Urambo.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (mwenye shati la bluu) akikagua mradi wa umeme katika Kijiji cha Mabundulu wilayani Urambo, Mkoa wa Tabora wakati alipofika kijijini hapo kuwasha umeme. Wengine ni viongozi mbalimbali kutoka wilayani Urambo na wananchi.
………………..
Na Hafsa Omar, Tabora
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amemuagiza Meneja wa Shirika la umeme Tanzania (TANESCO), Mkoa wa Tabora, kuwa vijiji vyote vinavyozunguka mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Urambo, vipatiwe umeme ndani ya miezi Sita.
Alisema hayo Agosti 24, 2019 wakati alipofanya ukaguzi kwenye mradi wa Ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Urambo, Tabora hadi Kigoma na kuzungumza na wananchi katika kijiji cha Uhuru kata ya Vumilia wilayani humo.
Akizugumza na wanachi wa kijiji hicho, Waziri Kalemani alisema “huwezi ukajenga kituo cha kupoza hapa, halafu vijiji vilivyozunguka hapa visiwe na umeme, kwahiyo vijiji vyote vinavyozunguka kituo hiki natoa miezi Sita viwe vimeunganishiwa umeme.”
Aidha, Dkt. Kalemani aliwapongeza wananchi wa Wilaya hiyo kwa uvumilivu wao katika kipindi chote kwa kutopata umeme wa uhakika na kueleza kuwa “mmehangaika miaka mingi lakini, Serikali yenu ni sikivu ndiyo maana sasa inaleta umeme imara unaotabirika, na ninampongeza sana Mheshimiwa Rais Magufuli kwa kutoa fedha za kutosha za kujenga mradi huu.”
Vilevile Dkt. Kalemani alisema kukamilika kwa mradi huo kutaokoa pesa nyingi zinazotumika kununua mafuta kwa ajili ya kuendeshea mitambo ya umeme.Alitoa mfano kuwa, Mkoa wa Kigoma unatumia takribani shilingi bilioni 1.1 kwa mwezi kuendesha mitambo ya mafuta ambapo kwa mwaka inatumika bilioni 13.2 hivyo umeme wa gridi utaokoa fedha hizo.
Alieleza kuwa, mradi huo wa njia ya kusafirisha umeme unatekelezwa na TANESCO wenyewe na hawatatumia wakandarasi wa nje ya nchi.
Katika ziara hiyo, Dkt Kalemani aliwasha umeme katika kijiji cha Madundulu tarafa ya Usoke, wilayani Urambo.
No comments: