Unavyoweza kujipaisha kithamani kwa mpenzi wako -2

MARAFIKI tunaendelea na mada yetu iliyoanza wiki iliyopita ambapo tunaangalia namna ambavyo unaweza kujipandisha thamani yako kwa mwenzi wako.  Tayari tumeshaona mambo kadhaa wiki iliyopita, leo tunaendelea pale tulipoishia. Marafiki, ukweli ni kwamba ni rahisi zaidi kulinda thamani yako kuanzia mwanzo wa uhusiano wenu.

Ikiwa tayari mmeshakomaa halafu tatizo hilo likajitokeza, hutumika nguvu nyingi zaidi kulirekebisha kuliko kujizatiti kuanzia mwanzo wa uhusiano. Ni mambo gani ya kuyazingatia mwanzo wa uhusiano? Tuendelee hapa chini.

CHUNGA KAULI ZAKO

Naomba ieleweke wazi kuwa mada hii zaidi ni maalum zaidi kwa wanawake. Kitu muhimu cha kwanza kabisa kwa mwanamke ambaye anataka kuilinda thamani yake kwa mpenziwe ni kupima sana kauli zake.

Acha kuropoka hovyo, pima maneno yako na ikiwezekana kama unadhani kuna jambo huna hakika nalo usizungumze kabisa. Katika eneo hili, uwe makini zaidi mnapokuwa na watu wengine. Kama mwanamke usiwe mchangiaji hoja sana. Utulivu wako unaweza kuwa silaha kubwa ya kukufanya ubaki na thamani yako kama mwanamke unayejitambua.

USIRUHUSU MAPENZI

Msichana mwenye kujitambua na kufahamu thamani yake sawasawa hawezi kuruhusu mwili wake ujulikane na mwanaume harakaharaka. Onesha unajitambua na usikubali kirahisi kuuacha mwili wako uchezewe.

Mpe hoja; kwanza mapema, hajakuoa wala kukuchumbia, haraka ya nini? Wakati unawaza kuhusu kutoa penzi lako, lazima ufikirie kuhusu athari zinazoweza kukupata kwa kukurupukia mapenzi. Mwanaume ambaye bado hamjachunguzana na huna hakika naye ya kutengeneza maisha, kichwani mwake hakuweki kwa asilimia kubwa. Ukumbuke kwamba, ukipata matatizo yoyote – binafsi au yanayosababishwa na uhusiano wenu, anakuwa hana uwajibikaji wa asilimia kubwa kwa tatizo hilo. Utabaki wewe na matatizo yako!

Mwingine anaweza kujiuliza; itawezekana kweli kuwa na uhusiano bila kukutana faragha? Ni kweli kuna ugumu katika kipengele hiki hasa kwenye dunia tuliyonayo, lakini asikudanganye mtu, ukiweza kusimamia kipengele hiki, thamani yako itapanda maradufu na kudumu kwa mpenzi wako. Tafiti mbalimbali zinaonesha kwamba, wanawake ‘wagumu’ zaidi kukubali kutoa tendo la ngono au kukataa kabisa mpaka ndoa, huwa na nafasi kubwa zaidi ya kuingia kwenye ndoa.

Mtaalam wa Saikolojia katika Uhusiano na Ndoa, Dk Dennis Robbinson wa Uingereza, anaeleza katika kitabu chake cha Love & Life (Mapenzi na Maisha) kuwa wanaume ‘waoaji’ huvutiwa zaidi na wanawake ambao ni wagumu kukubali kuachia miili yao ichezewe na wanaume.

“The main point here is individualism; men like to have women to themselves only without sharing with anybody. To them, having easily accepted for making love means even if they marry such women, they could be easily giving love out of marriage than those who hardly accept such approaches or those who completely refuse such approaches,” anaeleza Dk Robbinson katika sehemu ya kitabu hicho.

Kwa tafsiri isiyo rasmi, Dk Robbinson anasema, hoja kubwa (katika suala la kuharakisha mapenzi) ni ubinafsi; wanaume wanapenda kuwa na wanawake wao peke yao bila kuchangia na mtu. Wanaamini kukubaliwa haraka faragha humaanisha kuwa hata wakioa ni rahisi zaidi wanawake hao kutoa penzi nje ya ndoa kuliko wale wagumu au wanaokataa kabisa.

Wakati fulani niliwahi kukutana na msichana mmoja ofisini kwangu akihitaji ushauri. Jambo lililokuwa linamsumbua ni kichekesho. Alikuwa akilalamilikia kitendo cha mpenzi wake (rafiki tu) kukataa kupokea simu na kujibu meseji zake, wakati mwingine akifanya hivyo huwa kwa kuchelewa sana. Alisema kwamba, kinachomshangaza zaidi (eti) hata anapomhitaji mwanaume wake faragha humpiga chenga. Anaamini tendo la ngono kwa rafiki yake ni halali yake na akilikosa ni sawa amedharauliwa!

Nilimshangaa sana, lakini ilibidi nifanye kazi yangu ipasavyo. Nilitumia saa mbili kuzungumza naye. Alinieleza mengi, lakini kubwa ni kwamba, yule bwana alimshamchoka! Dalili zote zilionesha kwamba, hafikirii kuwa naye katika ndoa kama alivyokuwa akiwaza mwanzoni. Nadhani kuna kitu umekipata hapo. Wiki ijayo tutaendelea na mada yetu, usikose Alhamisi ijayo.

Joseph Shaluwa ni mshauri wa maisha, uhusiano na ujasiriamali anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vingi, kikiwemo Maisha ya Ndoa kinachopatikana kwa oda. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

The post Unavyoweza kujipaisha kithamani kwa mpenzi wako -2 appeared first on Global Publishers.

No comments: