Tatizo la mtindio wa ubongo kwa watoto
MAMBO mengi yamesemwa kuhusu tatizo la mtindio wa ubongo kwa watoto, hali ambayo imekuwa ikisababisha jamii mbalimbali kuwanyanyapaa na hata kuwabagua wale wenye tatizo hilo. Kitaalamu, mtindio wa ubongo unaelezwa kuwa ni hali inayompata mwanadamu baada ya ubongo wake kushindwa kufanya kazi katika utaratibu wa kawaida.
Kimsingi, tatizo hili ni uwezo wa ubongo kutokukua vizuri na kushindwa kufanya kazi yake katika mazingira yake ya kawaida. Mtu mwenye uwezo mdogo wa kufikiri, si kwamba ana matatizo ya akili ama mtindio wa ubongo. Mtindio wa ubongo unaweza kusababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo ubongo kuathirika wakati wa kuzaliwa, na hata maisha ya utotoni.
Yapo mambo matatu yanayosababisha matatizo kwenye ubongo wa mtoto ambaye hajazaliwa mfano ugonjwa wa down syndrome hujitokeza baada ya matatizo katika vinasaba kutokea ambayo baadhi ya matumizi ya dawa, husababisha mabadiliko katika vinasaba kama vile dawa za kunywa, ulevi kupindukia (fetal alcohol syndrome) na kuwa na mwili wenye afya dhaifu kitaalamu huitwa fragile X.
Viasili wakati mwingine huwa ni matokeo ya mtindio wa ubongo. Hali hiyo hutokana na asili ya kifamilia kuwa inapotokea mmoja wa wanafamilia wana asili na tatizo la mtindio wa ubongo, basi wengine miongoni mwao watapata tatizo hilo. Pia matumizi ya dawa kali anazotumia mama wakati wa ujauzito, matumizi ya dawa za kulevya, pombe, hali ya hewa, au hata ajali husababisha mtoto mchanga kupata mtindio wa ubongo.
Pombe ina athari kubwa na mbaya hasa kwa wajawazito na matatizo wanayopata yanafahamika kitaalamu kama Fetal Alcoholic Syndrome (FAS) na watoto wengi wanaozaliwa na tatizo hili wanakuwa na nyuso ambazo siyo za kawaida (facial deformities). Kwa mfano, watoto hawa wanaweza kuwa na pua bapa na macho yaliyoingia ndani, kichwa kidogo au kupata matatizo ya kusikia na kutokuwa na uwezo wa kusoma.
DALILI ZA MTOTO KUWA NA MTINDIO
Kwanza, mtoto haonyeshi dalili yoyote ya kulia au anaweza kulia kwa kiasi kidogo, huchelewa kutembea na hata kuongea, haonyeshi kuvutiwa na mazingira yanayomzunguka, kwa maana kwamba hata kama kuna vitu vya kuchezea hawezi kujishughulisha navyo.
Dalili nyingine ni mtoto kuwa mgumu kufundishika na hata kujifunza kusoma huwa ni kazi ngumu ukilinganisha na watoto wa rika lake, hawezi kula mwenyewe, kuvaa mwenyewe au kujifunza kutumia choo. Zipo dalili nyingi zinazoweza kujitokeza na mara nyingi zinatambuliwa na madaktari maalum wa watoto.
Watoto wenye matatizo hayo wako wa aina mbili, wapo wenye ulemavu wa akili na wenye mtindio wa ubongo kwa wakati mmoja. Aina hizo zinatofautiana; mtoto aliyeharibika mota ya ubongo kwa kiasi kikubwa hupatwa na mtindio wa ubongo tu.
Kama mtoto atakuwa ametindia ubongo upande wa kushoto, madhara yataonekana upande wa kulia kwa mtoto kuburuza mguu na mkono kutofanya kazi na hivyohivyo endapo itatokea kwa upande mwingine, wakati mwingine husababisha ugonjwa wa kifafa kwa mtoto.
Tatizo lingine linakuja, ikiwa mota ya fahamu haikuharibika, basi mtoto atapatwa na ulemavu wa viungo. Mitindio ya ubongo kwa watoto wakati mwingine chanzo chake ni uvutaji sigara kwa mjamzito kwani pia husababisha mtoto kuzaliwa njiti, mtoto kuwa na kichwa kidogo, na kutounga uti wa mgongo.
Kisababishi kingine cha mtindio wa ubongo ni pale mama anapochelewa kupata huduma ya uzazi anapofikia hatua ya kujifungua ama wauguzi kushindwa kuchukua hatua za haraka baada ya kubaini njia ya uzazi kushindwa kufunguka. Watoto wengine wanaopata tatizo hili ni wale ambao wamezaliwa na mzazi mwenye umri wa zaidi ya miaka 35. Mwanamke ajiepushe kuzaa akiwa na umri wa zaidi ya miaka hiyo.
USHAURI
Utafiti uliofanywa na wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Emory cha Atlanta, Marekani katika Kitivo cha Dawa, unabainisha kuwa baadhi ya watoto wenye mtindio wa ubongo wanafundishika, wanaweza kubadilika, iwapo tu watafundishwa kwa makini na utulivu.
Mtu anayemfundisha mtoto wa aina hii inashauriwa kuwa hatakiwi kuwa na hasira, pia inashauriwa kuwapongeza wanapofanya vizuri japo kidogo.
Watoto wa aina hii inashauriwa wapewe nafasi ya kujenga urafiki na watoto wenzao wa rika lao, wasitengwe, wachanganywe na wanafunzi wenzao wasio na matatizo ya akili, japo hata kwa nusu siku. Utaratibu huu hujulikana kitaalamu, mainstreaming.
The post Tatizo la mtindio wa ubongo kwa watoto appeared first on Global Publishers.
No comments: