Man United chali, Chelsea wapeta

 

WAKATI Manchester United ikipigwa nyumbani, wenzao Chelsea walishinda kwa mara ya kwanza mechi ya Ligi Kuu England jana. Manchester United ilijikuta ikipokea kipigo cha mabao 2-1 kwenye uwanja wao wa Old Trafford kutoka kwa Crystal Palace.

 

Kufungwa huko kwa mara ya kwanza kwa Manchester United kumeifanya kubakia na pointi nne, ambapo imefikiwa pointi hizo na Crystal Palace.

Muuaji wa Manchester United kwenye mechi ya jana alikuwa beki wa Crystal Palace, Patrick Van Aanholt, ambaye aliunganisha wavuni pasi ya Wilfried Zaha wakati huo matokeo yakiwa 1-1.

Jordan Ayew ndio alipachika bao la kuongoza la Crystal Palace baada ya kuunganisha wavuni pasi ya kichwa ya Jeffrey Schlupp katika dakika ya 31.

Manchester United ingawa ilikuwa na bahati mbaya ya kuendelea na mkosi wa kukosa penalti kufuatia straika wao Marcus Rashford kupiga ikagonga mwamba katika dakika ya 68.

Rashford alikosa penalti ikiwa siku chache baada ya mwenzake Paul Pogba kupoteza naye kwenye mechi dhidi ya Wolves, ambapo alishutumiwa kwa kung’ang’ania kupiga badala ya kumwachia Rashford.

 

Hata hivyo, Manchester United ilisawazisha kupitia kwa winga wake Darren James katika dakika ya 88 baada ya kupokea pasi ya Anthony Martial. Chelsea nayo ilipata ushindi wake wa kwanza kwenye ligi baada ya kuiliza Norwich City mabao 3-2 jana kwenye Uwanja wa Carrow Road.

 

Tammy Abraham alipachika mabao mawili ya Chelsea katika dakika za 3 na 68 wakati jingine likipachikwa na Mount Mason mnamo dakika ya 17. Mabao ya Norwich City yalifungwa na Todd Cantwell na Teemu Pukki katika dakika za 6 na 30.

The post Man United chali, Chelsea wapeta appeared first on Global Publishers.

No comments: