MAGARI YANAYOTUMIA GESI YAONGEZEKA HAPA NCHINI
Na Veronica Simba – Dodoma
SERIKALI imebainisha kuwa matumizi ya gesi asilia katika magari nchini yamezidi kukua ambapo kwa sasa idadi imefikia 210 kutoka 65 yaliyokuwa yakitumia nishati hiyo, mwaka 2017.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio, jijini Dodoma, leo Agosti 21, 2019 wakati akiwasilisha taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kuhusu hatua zilizofikiwa katika kuandaa moduli ya miradi ya bei ya gesi asilia, uuzaji na usambazaji wake majumbani na viwandani.
Akieleza zaidi, Dkt. Mataragio alisema kuwa kutokana na ongezeko hilo, kituo cha majaribio kilichopo Ubungo Dar es Salaam, kinashindwa kuhimili matakwa ya matumizi hivyo shirika limejipanga kujenga kituo kikubwa eneo la Sam Nuyoma jijini humo, ili kuondoa changamoto husika.
“Kituo hicho kinachotarajiwa kukamilika Oktoba 2020, kitatumika kujazia gesi katika magari pamoja na kupeleka gesi maeneo ambayo miundombinu ya mabomba ya gesi bado haijafika, yakiwemo maeneo ya viwanda Kigamboni na Kibaha pamoja na maeneo ya Feri na Muhimbili.”
Aidha, alieleza kuwa, sambamba na ujenzi wa kituo husika, shirika limetangaza fursa kwa kampuni binafsi kuuza gesi kwa rejareja kwa watumiaji wa nishati hiyo katika magari nchini. Aliongeza kuwa, jumla ya shilingi bilioni 16.6 zimetengwa kwa ajili ya vituo vya kuongeza mgandamizo wa gesi (CNG) na kujazia gesi katika magari.
Ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za uwezeshaji matumizi ya gesi katika magari nchini, Dkt. Mataragio alisema TPDC inalenga kuupatia gesi asilia mradi wa mabasi ya mwendokasi (DART), ambapo kwa kuanzia, kituo cha kujazia gesi kwenye magari kitajengwa eneo la DART, depoti ya Ubungo na kinatarajiwa kukamilika Oktoba, mwakani.
Alisema, shirika limekubaliana na DART kuwezesha kuweka vituo maalumu vya gesi katika depoti ya Gongo la Mboto na Mbagala ili kupunguza gharama za uendeshaji wa miradi ya DART na kuongeza matumizi ya gesi asilia.
“Miundombinu hii pia itakuwa na matoleo ya kuwezesha usambazaji wa gesi asilia kwa matumizi ya viwanda na majumbani katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam,” alisema.
Akizungumzia kuhusu mikakati mingine inayofanywa na shirika hilo katika kuwezesha ongezeko la matumizi ya gesi asilia nchini, Dkt. Mataragio alisema TPDC imepanga kuendeleza miundombinu ya usafirishaji gesi asilia ikiwemo kujenga bomba la gesi kutoka Tegeta hadi Bagamoyo katika eneo la viwanda.
Aidha, alisema shirika limepanga kujenga bomba la gesi kutoka Dar es Salaam hadi Tanga ambalo litakuwa na matoleo ya kwenda mikoa mingine pamoja na nchi za jirani kulingana na Mpango kabambe wa Matumizi ya Gesi Asilia Nchini (NGUMP).
Katika uwasilishaji huo wa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Ujumbe wa serikali uliongozwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu. Wengine walioshiriki ni viongozi na wataalamu mbalimbali kutoka wizarani, TPDC na taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio (kushoto) akikagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia kuwaunganishia wateja wa viwanda maeneo ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani, hivi karibuni.
No comments: