Kupanda na Kupotezwa Coutinho Barcelona
PHILIPPE Coutinho amekimbilia Bayern Munich ili kuokoa soka yake baada ya kushindwa kutamba Barcelona. Kiungo huyo wa Kibrazili aliamua kuondoka Liverpool katika kipindi ambacho soka yake ipo juu. Barcelona ilijitosa kulipa ada ya pauni milioni 142 (Sh, bilioni 395) mwezi Januari 2018 ili kumchukua kutoka Liverpool.
Ametua Bayern baada ya kuwepo taarifa alikuwa anafukuziwa pia na timu za Arsenal na Tottenham Hotspur. Coutinho ameamua kwenda zake kucheza kwa mkopo Bayern Munich ili angalau kuweka sawa kipaji chake.
Bayern imelipa kiasi cha pauni milioni 7.78 (Sh. bilioni 21) ili kufanikisha dili hilo la mkopo, ambapo wakiridhika naye basi watatakiwa kulipa kiasi cha pauni milioni 110 (Sh. bilioni 306) ili kumsajili moja kwa moja.
Kimsingi Coutinho kwa sasa ameshuka kiwango tofauti alipokuwa anatisha wakati akiwa Liverpool. Barcelona ilimnunua ikiamini imepata mbadala wa kiungo mchezeshaji Andres Iniesta, ambaye alikuwa anajipanga kuondoka kwenye klabu hiyo. Hata hivyo, hakuaminika kwa kocha wa Barcelona, Ernesto Valverde, ambaye alikuwa hampi nafasi.
Coutinho, ambaye alianzia soka yake katika klabu ya Vasco, aliibukia Ulaya mwaka 2008 wakati aliposajiliwa na Inter Milan akiwa na umri wa miaka 16. Hata hivyo, alirudishwa kwenda kucheza kwa mkopo Vasco da Gama ili kupandisha kiwango chake.
Alirudi tena Inter Milan mwaka 2010 ambako hakuweza kupata nafasi katika kikosi cha Inter na badala yake akatolewa kwa mkopo kwenda Espanyol, ambayo wakati huo ilikuwa inanolewa Mauricio Pochettino katika msimu wa 2011/12. Liverpool iliamua kujitosa kumchukua baada ya Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo, Damien Comoli kuwa ametonywa na kocha wa zamani wa timu hiyo, Benitez ikamsajili mwaka 2013.
Alipotua Liverpool, mambo yalimnyookea Coutinho kwani akaibuka kuwa mfungaji na mpishi wa mabao tegemeo wa Liverpool. Baada ya kung’ara Liverpool, ndio Barcelona na Real Madrid wakaanza fujo zao za kumwania kiasi cha kumvuruga kichwa Coutinho.
Mwaka 2017, Barcelona ilitaka kumchukua baada ya kutoa ofa ya pauni milioni 72 (Sh. bilioni 200) ambazo zilikataliwa na Liverpool.
Klabu hiyo haikukata tamaa bali ikatoa ofa nyingine mbili ambazo zilikataliwa na Liverpool iliyotaka dau la pauni milioni 183 (Sh. bilioni 509) Hata hivyo, katika kipindi wanakataa ofa za Barcelona walikuwa wapo bize wanamshawishi Coutinho abakie kwenye timu yao. Coutinho hakufurahishwa na kitendo hicho akaamua kuwasilisha maombi ya kuondoka Liverpool mwaka 2017.
Aliuzwa kwa ada ya pauni milioni 142 mwaka 2018 baada ya kocha Jurgen Klopp kuchoshwa na mambo yake. Kutua Barcelona Mashabiki wa Barcelona walimpokea kwa matumaini makubwa kuwa angeziba mapengo ya Neymar aliyekuwa amesepa zake na Iniesta, ambaye naye alikuwa mbioni kuondoka.
Coutinho akaanza kibarua cha kuzoea mazingira mapya na mambo yakaanza kuwa magumu baada ya kuwa anapangwa kwenye wingi wakati yeye alikuwa amezoea kucheza kama namba 10. Namba 10 wa Barcelona anaeleweka kuwa ni Lionel Messi, ambapo sasa Coutinho ikabidi aanze kuzoea nafasi ya pembeni.
Huo ndio ukawa mwanzo wa kupotea kwa Coutinho na matokeo yake amepachika mabao 21 katika mechi 75 alizochezea timu hiyo. Kufuatia hali hiyo, uongozi wa Barcelona umeona ni bora kuangalia uwezekano wa kuachana naye kutokana na kutofurahishwa na kiwango chake.
Mashabiki walio wengi wa Barcelona nao walianza kuona bora Coutinho aondoke baada ya kuchemsha. Coutinho kwa sasa anakabiliwa na changamoto kubwa ili kuweza kuzindua soka yake akiwa Bayern na kurud isha makali yake ya zamani.
The post Kupanda na Kupotezwa Coutinho Barcelona appeared first on Global Publishers.
No comments: