WAKIMBIZI KIGOMA WAIOMBA SERIKALI KUWATAFUTIA NAFASI ZA MASOMO ELIMU YA JUU WANAFUNZI WANAOMALIZA KIDATO CHA SITA
Moureen Rogath, Kibondo
Wakimbizi kambi ya wakimbizi Nduta iliyopo wilayani hapa mkoani Kigoma wameiomba serikali ya Tanzania kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi Duniani(UNHCR), kuwatafutia nafasi za kusoma elimu ya chuo kikuu kwa wanafunzi wakimbizi wanaomaliza kidato cha sita.
Wakizungumza jana kambini hapo katika maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani ambayo hufanyika Juni 20, kila mwaka, wamesema watoto wao wengi wanamaliza kidato cha sita lakini wameshindwa kuendelea na elimu ya juu.
"Hakuna chuo hapa Tanzania ambacho watoto wakimbizi watamaliza kidato cha sita na kwenda kusoma huko,tunaomba serikali itusaidie kwani tunatamani kuona watoto wetu wanafika mbali na kutimiza ndoto walizonazo katika maisha yao,”alisema Mkimbizi Paulo Bandondee,
Mwenyekiti wa kambi ya Nduta, Habarugira Godasi alisema wanatamani kurudi nchini kwao lakini kutokana na kupata taarifa ya kutokuwepo kwa amani wanashindwa kurudi.
“Tunatamani kurudi nyumbani na kwenda kutumikia nchi yetu lakini hatuwezi kurudi mpaka tutakapo hakikishiwa kuwa kumetulia kwani vyombo vya habari vya nchini kwetu vinatangaza bado hali sio nzuri,”alisema Godasi.
Aidha Shimiriamana Erick ameiyomba serikali ya Tanzania kuwavumilia na kuwapa huduma kwa kipindi ambacho wanakaa katika nchi yao huku akidai kuwa kuna siku amani itapatikana nchini mwao na watarejea.
Mkuu wa kambi ya wakimbizi Nduta kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani (MHA), Barnabas Kipii , amewataka wakimbizi kufuata sheria zilizowekwa na kutojihusisha na vitendo vya kiuhalifu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa wilaya ya Kibondo Luis Bula , Katibu tawala wa wilaya hiyo Ayubu Sebabili, amewataka wakimbizi wa Burundi kuwa tayari kurejea kwao kwa hiyari kwani wanazo taarifa kuwa ya kuwepo kwa amani."Niwaombe mashirika yanayohudumia wakimbizi kambini hapa kuangalia upya swala la kuwabadilishia chakula, kutoakana na kulalamika kuwa mmechoka kula ugali na njegele kila siku,”alisema Bula.
wakilishi wa UNHCR Barb Wigley alisema wanaishukuru serikali ya Tanzania na mkoa wa Kigoma kukubali kuwapokea na kuwapa hifadhi wakimbizi wa kutoka Burundi na Demokrasia ya Congo (DRC).
“Asilimia 80 ya ya wakimbizi wanaishi katika nchi za jirani na nchi zao, ni kazi kubwa ambayo nchi hizo zinazo wasaidia ikiwemo Tanzania ambayo imehifadhi wakimbizi 300,000 kutoka Burundi na DRC,”alisema Wigley.
Wakimbizi kambi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo mkoani Kigoma , wakiwa katika maandamano ya Maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani, yanayofanyika june 20 kila mwaka.picha zote na Moureen Rogath.
No comments: