MBUNGE KISHIMBA AIBANA SERIKALI 'MAITI KUTOZWA FEDHA' HOSPITALI

*Ataja sababu za wagonjwa kukimbilia kwa waganga wa kienyeji , aomba uwepo msamaha 

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

MBUNGE wa Kahama Mjini, kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) Jumanne Kishimba ameliambia Bunge anasikitishwa na tabia iliyopo kwenye hospitali za Serikali na zile za misheni ya mgonjwa anapofariki duniani kudaiwa deni la matibabu ndipo mwili uchukuliwe na ndugu.

Amefafanua kibaya zaidi ndugu wanapokuwa hawana fedha hizo, mwili wa marehemu unazuiliwa hadi deni lilipwe, hali ambayo ameitaka Serikali kupitia Wizara ya Fedha kuangalia na ikiwezekana kufuta msamaha wa madeni ya matibabu.

Kishimba ameyasema hayo Bungeni Mjini Dodoma wakati anachangia mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali ambapo amesema kuwa imefikia hatua ya miili ya marehemu kuzikwa na hospitali na kusababisha ndugu kutofahamu ilipozikwa maiti na wakati mwingine inazikwa kama mbwa.

Ameliambia Bunge kuwa wabunge walioko bungeni wote ni maiti na marehemu watarajiwa ila haijulikani muda wala saa.

 Wakati Kishimba anazungumza kuhusu hja yake, Naibu Spika Dk.Tulia Ackson alimtaka mbunge huyo kukaa chini na kisha akatangaza kumuongeza muda wa kuzungumza.

"Waheshimiwa wabunge kwa mujibu wa Kanuni ya 28 fasili ya tano naongeza muda wa 

nusu saa ili mheshimiwa Kishimba aweze kumaliza mchango wake,"alisema Dk.Tulia.

Hivyo wakati Kishimba anazungumza amesema kuwa "Ukiangalia kwenye bajeti yetu tumesamehe unga  wa keki, lakini tunatoza tozo la maiti kwenye mochwari. Nakuomba Waziri wa Fedha au Naibu Waziri wa Fedha, ebu rudisha hiyo kodi ya unga wa keki  ili tufute tozo la mochwari kwa maiti."

Amefafanua asilimia 95 ya vifo vinatokana na kuumwa na kuumwa kwenyewe mara nyingi 
kunakuwa ni kwa muda mrefu. Alisema mtu akiugua muda mrefu, anakuwa amedhoofika kiuchumi  na kiafya.

Ameongeza kwa kueleza kuwa leo hii mgonjwa anafariki hospitali inatoa bili ya Sh.500,000, anazipata wapi mheshimiwa 

Spika? Ameisha kufa na wachangiaji wengi humu wamesema, Watanzania wote wanalipa kodi, wanakunywa bia, wanavuta sigara...wanafanya shughuli zote.

Amehoji kwa nini Serikali isimsamehe bili mtu aliyefariki halafu hizo fedha zipelekwe katika keki na kwamba ni hatari na inaonekana  wanaotengeneza bajeti ni vijana waliopo 
Oysterbay."Nadhani walifikiri keki ni kitu cha maana sana wakashindwa kuelewa kuwa kuna shida nyingi kule kijijini.

"Naibu Spika alikuwa Kahama hivi karibuni na zile nyumba za nyasi ulizoziona ukiwa njiani ni za waganga wa kienyeji. Kwa waganga wa kienyeji ukipeleka mgonjwa na kwa bahati mbaya akafariki, hawaombi fedha. 

"Badala yake wanakusaidia kabisa na sanda. Inawezekanaje sisi Serikali tumdai mtu aliyefariki, halafu tukatalie maiti?" Amehoji na kuongeza; 

"Bahati mzuri Msigwa (Pater) ni mchungaji na Mama Rwakatare (Getrude)  wangetusaidia sana, maana yake turuhusu watu wakafanye maombi huko kwenye makaburi ya Serikali, watu wajue makaburi ya ndugu zao, baada ya miaka 10 watoto wakipata hela wakachukue mifupa ya wazazi wao wakazike upya."

Hivyo amesema hicho ni vizuri kikaangaliwa na Serikali kama ikiwezekana warudishe kodi ya unga wa keki. "Wanasema unga wa ngano unaotengeneza vyakula. Vyakula gani  mheshimiwa Naibu Spika? Ni keki na biskuti," amesema.

Mbunge huyo alichangia kuhusu mashine za X-ray na kusafisha figo ambapo amesema  daladala inauzwa kati ya Sh.milioni 50 hadi 100 kwa siku inaleta Sh. 50,000, Mashine ya X-ray  inauzwa Sh. milioni 40 hadi 100 mashine hiyo ikifanyakazi  kwa mgonjwa  kwa mgonjwa mmoja anatozwa kati ya sh. 100,000 hadi 200,000 kwa mtu mmoja.

Amehoji kama ni hivyo kwa nini Serikali isiruhusu watu binafsi wanunue X-Ray ili wazipeleke hospitali  ili gharama za X-Ray ipungue? Alisema anajua wataalamu wataleta maneno mengi ambayo yanahusu afya , lakini ni uongo kwani hata waganga wa kienyeji wanapewa kibali na Wizara ya Afya kuendesha shughuli zao na hawana elimu yoyote ya hospitali.

"Kule kwetu kanda ya ziwa, mgonjwa mahututi ndiye anapelekwa kwa mganga wa kienyeji 

ambapo hakuna choo, sasa iweje Serikali ikatae watu wanunue X-Ray wapeleke kwenye  hospitali?" Amehoji Kishimba.

Ameongeza kwenye nchi nyingine bili ya maji na umeme inamdhamini mtu hospitali na kwamba ikija bili ya maji na umeme, mamlaka husuka zinakaa  hospitali na kujadiliana namna ya kulipa deni la matibabu, hivyo watu wa hospitali wanaigiza madai yao humo na mtu anaanza kulipa kidogo kidogo.

"Mtu akilipa bili ya maji au umeme kinachukuliwa kiasi kidogo cha fedha kama ni  4,000 kinapelekwa hospitali, lakini mtu anakuwa amepona, kuliko sasa hivi kama hauna fedha ni tatizo sana,"amesema.

Hivyo amemtaka Waziri wa fedha kuliangalia hilo na kuhusu watu wasiokuwa na kadi za bima kukosa matibabu, Kishimba ameshaui hospitali zikubali hata kupokea kuku kutoka kwa wagonjwa ili mtu akishatibiwa zinauzwa ili kufidia gharama za matibabu.

"Wakati wakati wa mkutano wa Rais na wafanyabiashara kikubwa kilichokuwa kikilalamikiwa ilikuwa ni suala la uchunguzi baada ya mtu kuwa amemaliza kulipa kodi. Suala la kutafuta watu watakatifu yeye haliamini.

"Kwani hata dini ina miaka 2000 tangu Yesu aje, lakini watu hawajashika dini. Ili kumaliza mgogoro  unaosababisha matatizo TRA wanayo sheria inayohusu mtu ambaye  hakufanya mahesabu wamtoze kwa gharama ya mauzo, inawaruhusu wao kumchunguza yeye,"amesema.

Ameongeza Sheria hiyo iliachwa na mkoloni kwamba kama mtu hana vitabu analipa asilimia 2 ya mauzo yake, kwa hiyo kama mtu ameuza Sh. bilioni 1, asilimia mbili ni Sh. milioni 20.

"Hivyo kwa sababu asilimia 90 ya wafanyabiashara wa Tanzania elimu yao ni darasa la saba. wengine hawakusoma kabisa, inakuwa kazi ngumu sana utunze stoo ya mali, utunze stoo za karatasi na bado karatasi hizo hizo ukipeleka (TRA) unaambiwa hazifai,"amesema.

No comments: