MAHAKAMA KUU YA TANZANIA YAMTIA HATIANI RAIA WA KIGENI KWA KUKUTWA NA HATIA YA KUSAFIRISHA PIPI 56 ZA DAWA ZA KULEVYA AINA YA HEROIN
Na Karama Kenyunko, Blog ya Jamii
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu uchumi, imemtia hatiani raia wa Nigeria Christian Ugbechi baada ya kumkuta na hatia ya kusafirisha pipi 56 za dawa za kulevya aina ya heroin hydrochloride.
Uamuzi huo umefikiwa leo, Juni 19, 2019 na Jaji Sirrilius Matupa ambae amesema upande wa mashitaka katika kesi hiyo umeweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka kupitia mashahidi wake 11 na vielelezo 22 waliofika mahakamani hapo kuthibitisha mashitaka hayo, kuwa mshitakiwa ametenda kosa hilo.
Amesema pamoja na mshtakiwa kujitetea kwamba alifanyiwa upekuzi mara tatu na hakukutwa na kitu chochote na hivyo upande wa mashitaka ulipaswa kuleta ushahidi wa CCTV, haikuwa lazima kuwapangia upande wa mashitaka mashahidi wa kuwaleta na kwamba walikuwepo mashahidi wengine waliothibitisha mashitaka.
Amesema mkemia mkuu wa serikali katika uchunguzi wake, amethibitisha dawa za kulevya alizozichunguza ndizo alizokutwa nazo mshitakiwa huyo.
Kabla ya kusomwa kwa adhabu Jaji Matupa aliuliza upande wa mashtaka kama walikuwa na lolote la kusema ambapo Wakili wa Serikali, Constantine Kakula amedai kuwa hawana kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya mshitakiwa lakini wameiomba mahakama itoe adhabu kali iwe fundisho kwa watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Upande wa utetezi, Jeremiah Ntobesya aliomba mahakama kumpunguzia adhabu mteja wake kwa sababu ana mke na watoto wawili wanaomtegemea na pia mshtakiwa anasumbuliwa na matatizo ya moyo na kwamba amekaa gerezani kwa mwaka mmoja na nusu nankipindi hicho chote alikuwa na tabia njema.
Pia alisema, pamoja na kwamba kifungu cha sheria kinaamuru mshtakiwa kuhukumiwa kifungo cha maisha gerezani lakini siyo lazima, itolewe adhabu hiyo, mahakama inaweza kuamua vinginevyo.
Kutokana na ubishani wa kisheria juu ya adhabu anayopaswa kusomewa mshitakiwa mahakama imesema itamsomea mshitakiwa huyo adhabu yake, Juni 21, 2019 (Ijumaa).
Mapema katika ushahidi wake, askari wa upelelezi kutoka Kituo cha Uwanja wa ndege namba G 1782 D/C Peter alidai kuwa aliandika maelezo ya mshitakiwa huyo na katika mahojiano alimueleza kuwa amemeza pipi za dawa za kulevya.
Alidai baada ya kueleza hayo alimuweka mahabusu ili aweze kuzitoa na kwamba hadi Januari 30,2018 saa 10:30 jioni alitoa pipi 23 alizomeza.
Pia alidai walichukua kielelezo hicho na pipi nyingine zilizokutwa kwenye begi na kuzipeleka kwa Mkemia Mkuu wa serikali ambapo kwa pamoja zilikutwa na uzito wa gramu 947.17.
"Matokeo ya uchunguzi yalionesha kuwa pipi zote zilikuwa ni dawa za kulevya ambazo ni heroin hydrochloride zilizochanganywa na paracetamol metronidazole na papavirine," alidai Peter.
Mkuu wa Kituo cha Uwanja wa ndege, Inspekta Dickson Haule alidai siku ya tukio majira ya saa 14:00 mchana akiwa ofisini alijulishwa na askari huyo wa upelelezi kuwa kuna mtuhumiwa amekamatwa na dawa za kulevya.
Haule alidai baada ya taarifa hiyo alienda Ofisi ya Polisi Interpol walipokuwa na alishuhudia mtuhumiwa akipekuliwa ndipo aliona begi dogo la mgongoni kuna pipi 56 zikiwa zimeviringishwa ndani ya soksi mbili nyeusi.
Katika kesi hiyo, inadaiwa Januari 28, mwaka jana maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam, mshtakiwa alikutwa akisafirisha sha dawa za kulevya aina ya Heroine hydrochloride zenye uzito wa gramu 947.57.
RAIA wa Nigeria, Christian Ugbec akiwa katika kizimba cha Mahakama Kuu Tanzania Kitengo cha makosa ya Rushwa na uhujumu uchumi maarufu kama mahakama ya mafisadi, akisubiri kusomewa hukumu yake dhidi ya kesi ya kukutwa na dawa za kulevya aina ya Heroine Hydrochloride. Hata Hata hivyo, mshitakiwa huyo ametiwa hatiani na atasomewa adhabu yake Juni 21,2019.
No comments: