WAZIRI LUGOLA AIPA POLISI WIKI MOJA KUFANYA UCHUNGUZI, KUWAKAMATA WATUHUMIWA WA MAUAJI YA WANAWAKE MTO WA MBU MKOANI ARUSHA

Na Mwandishi Wetu, MOHA-Monduli

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ametoa wiki moja, Jeshi la Polisi kuhakikisha linafanya uchunguzi wa kina kwa kuwakamata watuhumiwa waliofanya matukio ya kikatili ya ubakaji na mauaji ya wanawake yaliyotokea Mto wa Mbu Wilayani Monduli, Mkoa wa Arusha.

Akizungumza na wananchi wa Mji mdogo wa Mto wa Mbu, wilayani humo, leo, kutokana na matukio hayo, Waziri Lugola amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, kushirikiana na Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo, na kusimamiwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, kuhakikisha uchunguzi wa kitelijensia unafanyika juu ya watu wanaohusika kufanya vitendo hivyo vya kikatili katika eneo hilo.

Lugola aliongeza kuwa, haiwezekani wananchi wa eneo hilo wawe wanaishi kwa wasiwasi, wanateswa, kuuawa na kudhalilishwa wakati Serikali ya Rais Dkt John Magufuli ipo, Polisi wapo, pamoja na wananchi wapo, kwa hatua hiyo lazima mauaji hayo yafikie kikomo.

"Ndugu wananchi Serikali ya Dkt Magufuli haiwezi kuchzewa hata kidogo, lazima tudhibiti hii taaruki, na tusipofanya hivi, hii hali itaendelea kushika kasi jambo ambalo Serikali haiwezi kukaa kimya,” alisema Lugola na kuongeza;

“Wakina mama wataisha kutokana na vitendo hivyo vya kikatili na lazima tuwe na uchungu sasa, Jeshi la Polisi lijipange vizuri kwa kufanya kazi ya weledi kwa muda wa wiki moja hakikisheni mnafanya kazi nzuri ipasavyo ili kuwatia mbaroni hao watuhumiwa na kufunguliwa mashtaka haraka iwezekanavyo,” alisema Lugola.

Lugola aliwatoa wasiwasi akina mama wa mji huo na kuwataka kuleta taarifa za siri kuhusiana na wahusika hao kwasababu hawatoki mbali bali katika mazingira hayo hayo wanayoishi.

“Mmependekeza mpige kura za kimya kimya kwa kuwa uwanjani mkiandika majina ya watuhumiwa, mkihofia mkipeleka taarifa Kituo cha Polisi kwa njia ya siri mnahofia mtakuja julikana, sijakataa njia mliopendekeza, lakini Polisi watafanya kazi hii ya kiitelejinsia hapa kwa umakini na watawakamata watuhumiwa,” alisema Lugola.

Lugola pia aliwataka wananchi hao kutoa ushirikiano wa kina kwa polisi hao wakati wanafanya kazi zao, pia aliwapa angalizo polisi hao wasije wakakurupuka wakati wanafanya uchunguzi huo, wasiwaonee wananchi, wahakikishe wanakua makini ili wasije wakawasumbua ambao wananchi ambao wanafanya shughuli zao za kibiashara.

Aidha, Mjumbe wa Kijiji cha Kigongoni, Kata ya Mto wa Mbu, Tarafa ya Manyara, Wilayani humo, Devotha Steven alisema wanaiomba Serikali iongeze nguvu katika kuwalinda wanawake wa Mto wa Mbu kwani vitendo vya kikatili vimekuwa vya kusikitisha na pia wanakosa amani popote wanapofanya shughuli zao za kutafuta ridhiki.

"Mheshimiwa Waziri, ninazungumza kwa machungu, kwanini tunateseka na Serikali ipo, tunaamini mtasambaratisha haya mauaji, nasema kwa uchungu yatima wanaongezeka, tunaomba tupige kura na wanachi waitwe kutoka tarafa ya Manyara na Makuyuni ili wahusika wapatikane na tunaomba ulinzi utolewe kwa wale wananchi wanaotoa siri walindwe," alisema Devotha.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Monduli, Julius Kalanga, alifurahia ujio wa Waziri huyo, na pia alimwomba kiongozi huyo kupitia Jeshi lake, wawakamate wahalifu hao ambao wanafanya vitendo vya kikatili, ili ukatili huo uweze kukomeshwa.

Waziri Lugola yupo Mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi ambapo anatembelea Wilaya zote za Mkoa huo akifuatilia utendaji kazi wa Taasisi zake zilizopo ndani ya Wizara yake.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia), akimsikiliza Mjumbe wa Kijiji cha Kigongoni, Kata ya Mto wa Mbu, Wilayani Monduli, Mkoani Arusha, Devotha Steven, alipokuwa anaiomba Serikali iwakamate watuhumiwa wa mauaji ya wanawake katika Kata hiyo. Lugola ametoa wiki moja, Jeshi la Polisi mkoani humo kufanya uchunguzi wa kina na kuwakamata watuhumiwa hao. 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia), akimpa maelekezo Kaimu Kamanda wa Polisi Arusha, Longinus Tibishubwamu (kushoto), kuwakamata watuhumiwa wa mauaji ya wanawake katika Kata ya Mto wa Mbu, Wilayani Monduli, Mkoani Arusha. Wapili kushoto ni Kamanda wa Polisi Wilaya ya Monduli, Gilbert Ngaizi, na wapili kulia ni Mkuu wa Kituo cha Polisi Mto wa Mbu, Peter Ngoro.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia), akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Mji wa Mto wa Mbu, wakati Waziri huyo alipohudhuria Sikukuu ya Maulidi iliyofanyika mjini humo, leo. Lugola aliwataka viongozi wa dini kuhubiri amani ili wananchi waache kufanya matukio ya uhalifu katika mji huo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

No comments: