TFF, Takukuru Wayafanyie Kazi Madai ya Zahera
KWA mara nyingine juzi Ijumaa mchana, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amerudia kauli yake ya tuhuma za rushwa kwenye Ligi Kuu Bara,anadai kuna timu kubwa inacheza mechi za timu nyingine. Kocha huyo licha ya kwamba hakutaja jina la timu husika lakini alidai kuwa kuna klabu moja tajiri inayohonga marefa na wachezaji wa timu pinzani kwenye mechi dhidi ya Yanga.
Zahera amedai kuwa timu hiyo imekuwa ikitoa kiasi cha fedha kwa waamuzi na wachezaji katika mechi zinazoihusisha Yanga. Akaenda mbali zaidi kwa kutolea mfano mechi yao dhidi ya Singida na ile JKT Tanzania ambazo zote zimechezwa ugenini.
Amedai hadharani kuwa uongozi wa timu moja kubwa uliwaahidi wachezaji wa Singida Sh10milioni kama wangeifunga Yanga na Sh5milioni kama wakipata japo sare. Akaenda mbali zaidi kwa kudai kwamba hali kama hiyo ilitokea pia kwenye mechi na JKT Tanzania mjini Tanga.
Anadai kwamba wamepewa ushahidi na wachezaji wa timu hizo ambao baadhi yao waliwahi kuichezea Yanga katika misimu ya hivikaribuni na wana mapenzi na Yanga.
Maoni yetu sisi ni kwamba tuhuma za Zahera ni nzito sana na hazipaswi kupuuzwa kwa maendeleo ya soka la Tanzania pamoja na kuhakikisha mambo yanakwenda kwa haki. Rushwa ni kitu kibaya sana kama kikiruhusiwa kustawi kwenye soka letu haswa katika kipindi hiki ambacho klabu nyingi hazina fedha.
Takukuru na TFF ni vyombo ambavyo vinapaswa kuyafanyia kazi kwa kina madai hayo ya Zahera na ikiwezekana hata yeye mwenyewe aitwe avisaidie vyombo husika kwa masilahi ya soka la Tanzania.
Siyo sahihi na wala haikubaliki kwenye soka klabu kuhonga waamuzi na wachezaji wa timu pinzani ili timu nyingine ifungwe. Hiyo ni rushwa mbaya kabisa ambayo kila mwanamichezo anapaswa kuipiga vita ndio maana tunasisitiza kwamba vyombo husika viongeze umakini na viingie kazini kufanya kazi yao kukomesha hayo.
Kama ni kweli hali hiyo ikistawi itaua kabisa soka letu na kila mara tutakuwa tunapata wawakilishi feki kwavile ushindani hautakuwepo. Tuache soka lichezwe na kila mtu mwenye uwezo ashinde kwa haki uwanjani bila matumizi ya rushwa au mambo mengine mbadala.
Hali ya kupenyeza rushwa kwa waamuzi kutazinyima haki timu zingine na kufanya ligi yetu kupoteza mvuto kwavile baadhi ya timu ndizo zitakuwa zinatamba tu na kufanya zinavyotaka haswa kwenye wakati huu ambao mashindano hayo hayana mdhamini mkuu. Tunakemea kwa nguvu rushwa michezo kwani kama ilivyo kwenye maeneo yote ni adui wa haki.
Tunavisisitiza vyombo husika kwenye Ligi Kuu Bara pamoja na mamlaka za Serikali zitoe macho mawili kwenye Ligi yetu ili kuhakikisha madudu kama hayo yanatokomezwa. Kila mmoja anapaswa kushinda au kushindwa kwa haki na si kwa shinikizo la mtu, kikundi au timu fulani yenye nguvu ya fedha.
Tanzania lazima tubadilishe fikra zetu na tucheze soka uwanjani. Madai ya Zahera yafanyiwe kazi kwa umakini yasipuuzwe au kuchukuliwa kama jambo jepesi.
The post TFF, Takukuru Wayafanyie Kazi Madai ya Zahera appeared first on Global Publishers.
No comments: