TAMASHA LA LADY IN RED KURINDIMA JUMAMOSI HII, LALENGA KUIBUA VIPAJI KWA VIJANA

* Waandaaji waishukuru Serikali kwa ushirikiano, yawahimiza vijana kujituma kwa kufanya kazi kwa bidii

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
JUKWAA la ubunifu nchini maarufu kama Lady in Red linatarajiwa kufanyika usiku wa jumamosi ya tarehe 18 mwaka huu ikiwa ni mara ya 16 tangu kuanza kufanyika kwake chini ya mwanzilishi wake Asya Idarous.

Akizungumza na waandishi wa habari muandaaji wa jukwaa hilo Didas Katona amesema kuwa jukwaa hilo ni kwa ajili ya kukuza sanaa na wabunifu chipukizi ili kuweza kuwasaidia kuweza kufikia malengo yao.

Amesema kuwa tamasha hilo litafanyika viwanja vya Escape One, siku ya tarehe 18 mwezi huu kuanzia majira ya saa moja jioni na kuwataka wapenzi wa  mitindo na ubunifu kujitokeza kwa wingi na kushuhudia wabunifu hao chipukizi watakavyoonesha ubunifu wa mavazi.

Katona amesema kuwa; " Walimbwende (models) 30 pamoja na wabunifu 10 watapata fursa ya kuonesha ubunifu wao na kujitangaza  na tuna imani watafika mbali zaidi kwa kuwa hali ya ubunifu kwa sasa ni nzuri na serikali inatuunga mkono, hivyo hii ni fursa kwao katika kujitangaza ili waweze kufika mbali zaidi" ameeleza.

Pia ameishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Joseph Magufuli, Baraza la sanaa la taifa (BASATA) na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kwa kuwa pamoja kuonesha ushirikiano wa hali ya juu na wasanii katika kuikuza na kuiendeleza sanaa nchini. 

No comments: