RC NDIKILO AWEKA JIWE LA MSINGI KITUO CHA AFYA IKWIRIRI
NA MWAMVUA MWINYI, RUFIJI
MKUU wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo ameweka jiwe la msingi katika kituo cha afya Ikwiriri, Rufiji, ambacho kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Charles Kabeho alikataa kuweka jiwe hilo July 2018,kutokana na mkanganyiko wa taarifa baina ya wilaya na mkoa .
Akizungumza baada ya kuweka jiwe hilo la msingi, Ndikilo alisema walichukua hatua ya kufanya uchunguzi kupitia vyombo vya dola na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) na kubaini hakuna wizi uliofanyika kwenye ujenzi huo.
"Kama kuna miundombinu kwa baadhi ya majengo haijakamilika iangaliwe namna ya kuikamilisha ,katika vituo vyote vya afya vinavyojengwa mkoani hapa "alisema Ndikilo .Aidha, alieleza wamepokea bilioni 8.2 kwa ujenzi wa vituo vya afya na bilioni 4.5 kwa ajili ya hospital tatu za wilaya.
Ndikilo, aliwaomba watumishi wa afya kutoa huduma bora ya afya kwa wananchi wanaofuata matibabu mbalimbali.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Rufiji, Mohammed Mchengelwa aliishukuru serikali, kwa kuimarisha sekta hiyo na imeshatoa zaidi ya sh. milioni 320 kuboresha sekta ya afya wilayani Rufiji.
Awali, mkuu wa wilaya ya Rufiji, Juma Njwayo alibainisha, wamejiridhisha kiwilaya hivyo kumuomba mkuu wa mkoa kufanya zoezi hilo.
No comments: