KILICHOTOKEA MAHAKAMANI RUFAA YA MBOWE NA MATIKO

LEO Jumatatu, Februari 18, 2019 kesi ya Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko kuhusu mapingamizi ya serikali dhidi ya kesi yao ya kupatiwa dhamana imesikilizwa kuanzia asubuhi  katika Mahakama ya Rufani.

 

Upande wa Mashtaka umewasilisha hoja mbili za rufaa katika Mahakama hiyo huku wakiomba rufaa hiyo iliyopo Mahakama hapo mbele ya Jaji Sam Rumanyika itupiliwe mbali kwa sababu haiendani na kifungu cha 362 (1) cha sheria ya Makosa ya Jinai sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo.

 

Kwa mujibu wa sheria hiyo rufaa ni lazima iambatanishwe na mwenendo wa kesi na uamuzi mdogo unaobishaniwa katika Mahakama Kuu lakini upande wa utetezi hawakufanya hivyo.

 

Rufaa hiyo ilikatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) dhidi ya Mbowe na Matiko akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu, kukubali kuendelea na usikilizwaji wa rufaa ya wabunge hao ya kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia dhamana.

 

Wakili wa Serikali Mkuu Faraja Nchimbi amedai leo mbele ya jopo la majaji watatu Stella Mgasha, Gerald Ndika, Mwanaisha Kwaliko wa Mahakama ya Rufani kuwa wanapinga uamuzi uliotolewa na Jaji Rumanyika katika rufaa hiyo uliotolewa Novemba 30, 2018.

 

Akitoa hoja ya kwanza ya Upande wa Masht5aka, wakili wa Serikali Nchimbi amedai Jaji Rumanyika alipotoka kisheria kwa kuipanga na kuiita kwa ajili ya usikilizwaji huku akijua rufaa hiyo iliwasilishwa kinyume na kifungu cha 362 (1) cha sheria ya mwenendo wa Makosa ya jinai sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo 2002. Pia wanadai Jaji Rumanyika alijipotosha kwa kushindwa kuwapatia haki ya kutosha ya kusikilizwa.

 

Kwa upande wa Wakili Peter Kibatala alidai kuhusu lalamiko la kuwa hawakupewa muda wa kutosha wa kusikilizwa, rufaa iliyopo Mahakama Kuu haikusikilizwa na kilichosikilizwa ni mapingamizi pekee.

 

Hata hivyo, Jaji Mgasha kwa niaba ya jopo amesema watazingatia hoja zilizowasilishwa na pande zote mbili na kwamba watatoa uamuzi katika tarehe itakayopangwa, lakini Kibatala amedai sababu za rufaa hiyo hazina mashiko hivyo aliomba Mahakama ya Rufani kuitupilia mbali rufaa hiyo ambapo Mbowe na Matiko wamerejeshwa Segerea.

The post KILICHOTOKEA MAHAKAMANI RUFAA YA MBOWE NA MATIKO appeared first on Global Publishers.

No comments: