BIBI TITI MOHAMED: MWANAMAMA SHUPAVU NA MPIGANIA UHURU HODARI ALIYETINGISHA NA KUHESHIMIKA AFRIKA MASHARIKI NZIMA!!!


1. Usuli:

1.1 TITI Kuzaliwa:
TITI MOHAMED SALUM MANDWAGA alizaliwa mwezi Juni 1926 jijini Dsm.

1.2 Wazazi Wa TITI: Baba yake aliitwa Bw. MOHAMED BIN SALIM na mama yake aliitwa Bi. HADIJA BINTI SALIM. Wazazi hawa walitokea Rufiji.

Baba yake alikuwa mfanyabiashara ya mbuzi na ng'ombe na mama yake alikuwa mkulima.

2. Elimu:

2.1 Baba Agoma TITI Asisome:
Baba yake alikataa katukatu kwamba TITI asisome shule kwa hofu angekuwa kafiri.

2.2 Mama Ampeleka TITI Shule:
Baba yake alifariki TITI akiwa na miaka 9 tu. Mamaye akatumia fursa hiyo kumpeleka TITI Shule ya Wasichana Uhuru ambako alisoma hadi darasa la 4.

3. TITI Aolewa na MHENGA akiwa na miaka 14 tu:
TITI aliolewa na mwanaume mzee ambaye angeweza hata kuwa baba yake wakati yeye akiwa binti wa miaka 14 tu. 

4. TITI Ajifungua Mtoto wa Kike:
TITI alijifungua mtoto wa kike aitwae HALIambaye alikuja kuolewa na MZEE IDD HAMIS, Mshambuliaji hatari wa Cosmopolitans, klabu ya kwanza kutwaa ubingwa TZ ambapo walikuwa wakiishi mtaa wa Skukuu na Udowe na kubahatika kupata watoto 3 wa kiume.

4. TITI Aachana na mumewe:
TITI aliachana na mume huyo kijeba ambaye alikuwa ni baba wa HALIMA , mume ambaye hakuwa chaguo lake.

5. TITI Awa Maarufu kwa ngoma za Maulid:
TITI alianza kuwa maarufu angali mdogo alipokuwa kiongozi wa ngoma za maulid ambazo zilimjenga uwezo wa kujiamini na hivyo akawa maarufu sana.

6. TITI Aolewa na BOI SELEMAN:
TITI aliolewa na dreva wa teksi aitwae Boi Selemani, baada ya ndoa yake ya kwanza kusambaratika.

6. TITI Ajiunga na TANU:
TANU ilizaliwa tarehe 7.7.1954. Wanachama wa mwanzo kupata kadi za TANU walikuwa NYERERE(Kadi na.1), A. SYKES Na.2, A. SYSKES No.3 D. AZZIZ No.4, DENIS PHOMBEAH No.5, DOME OKOCH Na.6, J. RUPIA Na.7.

Bw. BOI, mme wa TITI, alikuwa ni rafiki wa Bw. SCHNEIDER PLANTAN aliyekuwa mmoja wa viongozi wa TAA. Siku moja, Bw. PLANTAN alienda nyumbani kwa BOI na kumweleza kuwa ametumwa kumweleza TITI ajiunge na TANU.

BOI alikubali na akajinunulia kadi na.15 ya TANU na pia akamnunulia TITI kadi na.16. Jumla alitoa TZS 12/= kwani kila kadi iliuzwa TZS 6/=.Ndivyo walivyojiunga TANU. BOI pia alichangia TSH 10/= kwa ajili ya nauli ya Mwalimu NYERERE kwenda UNO (TSH 5/= kila mmoja).

7. TITI Asomba wamama Lukuki Kujiunga TANU!!!

Tarehe 8.7.1955, TITI akiwa Mwenyekiti wa Tawi la Wanawake wa TANU, alifanya mkutano mkubwa na kuvuna wanachama 400 na ndani ya miezi 3 tu akawa amepata wanachama 5,000:
"Nilizungumza na mama Swalehe Kubunju, Kiongozi wa "Tongakusema" na akawaita wakinamama wote wa Tongakusema. Nikakutana nao Livingstone street alikokuwa akiishi mama Kubunju ambaye alihimiza: -"Ewe mwanamke, TITI anakuita, TITI yuko hapa". Hivyo wamama wakawa wanakuja kirahisi. Wakija nikawa nawaambia tunataka uhuru lakini hatuwezi kuupata kabla ya kujiunga TANU. Wanawake ndio nguvu ya dunia, hawa wanaume wote tumewazaa. Nilizunguka Tanganyika nzima. Safari ya kwanza mikoani tulienda Tanga tarehe 1.1.1956 mimi, Bwana mkubwa na RAJAB DIWANI na tukazunguka Tanga nzima kwa siku 21. Tuliporudi Kamati Kuu ikanipa ruhusa ya kusafiri peke yangu. Pia nilifanya safari nyingi na OSCAR KAMBONA. Tukiwa na KAMBONA tulikuwa tukipita nyumba hadi nyumba, usiku na mchana".

8. TITI Atia Fora Mikutano ya NYERERE:
TITI ndiye aliyekuwa akiimbisha na kuhutubia kwanza kabla ya NYERERE kupanda jukwaani "kushusha" nondo. Kwa hakika, TITI alikuwa akikonga nyoyo kwa kiswahili chake cha pwani na nyimbo zake:  (Hongera mwanangu eeh na mi nihongere eeh hongera X 2) na (Mama Usungu, Mama Usungu X 2).

9. KENYA Wamuomba TITI "Awapige Tafu" Kudai Uhuru"
Uwezo mkubwa wa kushawishi na kujiamini kulifanya jina la TITI livuke mipaka ya Tanganyika. Wapigania uhuru wa Kenya TOM MBOYA, JARAMOGI OGINGA ODINGA nk walipopata sifa za TITI walituma ujumbe kumuomba aende Kenya kusaidia kuishawishi serikali ya mkoloni kumwachia huru JOMO KENYATTA.

TITI alienda Kenya na alitia fora sana maeneo ya Nairobi, Machakos, Kisumu na Mombasa.

Miaka michache baada ya KENYATTA kuachiwa, mara moja alikuja TZ. KENYATTA alihutubia mkutano mkubwa Jangwani akiwa na suaruali ya kodrai ya udongo na koti kubwa la kijivu huku akipeperusha usinga mweusi alimshukuru sana TITI kwa jitihada zake mujarab alipokuwa nchini Kenya.

Ni katika mkutano huu ndipo Mwalimu NYERERE alisema yuko tayari kuona Tanganyika inachelewa kupata uhuru ili Kenya ipate uhuru wake na ziweze kuungana.

10. TITI Amsindikiza NYERERE Airport kwenda UNO:
Tarehe 17.2.1955, TITI alikuwa mmoja wa wanaTANU waliomsindikiza NYERERE Airport kwenda UNO kuwaeleza kuwa "Tanganyika lazma kieleweke".

11. TITI Akumbana na changamoto kedekede:
Katika harakati zake za kuwashawishi wanawake na wanaume kujiunga na TANU, TITI alikumbana na changamoto lukuki. Kwanza aliambiwa ni mwizi wa waume za watu na pia akaambiwa anatafuna michango ya TANU:
"Kulikuwa na changamoto nyingi sana. Siku moja nilienda nyumba moja kuarifu mkutano wa TANU. Nikakuta wanawake wamekusanyika na kudai eti nimeenda kuiba waume wa watu. Lakini mmoja wao akawaambia huyu mama ndiye anaetangaza chama cha NYERERE nilimuona pia nyumba ya mbele, hana lengo baya".

12. BOI Alalamika kwa PLANTAN  kuwa Amegeuka Housegirl:
Mmewe TITI, BOI alilalamika vikali kwa PLANTAN kuwa TITI hatulii nyumbani kutokana na harakati za TANU hadi yeye kugeuka yaya wa kujipikia na kujifulia nguo na hakuona tena faida ya ndoa. BOI akamshutumu PLANTAN kwa kumuingiza TITI kwenye chama cha TANU. 

BOI pia wivu ulikuwa umerindima kwenye "medula oblangata yake" hadi akabwabwaja'- "TITI ni mwanamke wa kiislam, kasoma madrasa, kapanda jukwaani bila baibui. Hii si sawa kabisa".

13. Ndoa ya TITI Yaparaganyika Sababu ya Harakati za Kudai Uhuru:
Kutokana na mishemishe na safari zisizoisha za TITI, ndoa ya TITI ikaparanganyika kama alivyoelezea mwenyewe:
"BOI mwenyewe ndie aliyeniruhusu kujiunga na TANU na tena ndiye aliyeninunulia kadi ya uanachama. TANU pia ilimwandikia barua anisaidue mambo ya TANU.Lakini mwisho hizi safari zilimshinda. Nilikuwa nakaa nje ya Dsm hata kwa miezi 3 na nikirudi sikai hata siku 10, nasafiri tena. BOI akaniambia anataka kuoa mke mwingine. Nikamwambia sawa, niache na kazi yangu kwani nimeizoea. Kwahiyo BOI akamuoa Bi. KHADIJA lakini wakashindwana wakaachana. Nilifunga mizigo yangu nikaondoka kwa BOI".

TITI akaja kuolewa tena.

14. NYERERE na TITI "Waangusha" rhumba "La kufa mtu" siku ya uhuru".

Tarehe 9.12.1961, ilikuwa siku ya kipekee kwa Mwalimu NYERERE na TITI ambao kwa miaka kadhaa hapo nyuma walizunguka kila kona ya Tanganyika kuhimiza wananchi kujiunga na TANU na kudai uhuru.

Siku hiyo, Mwalimu NYERERE na TITI walikaa "High Table" na usiku wakiwa nadhifu walifungua muziki wa kuukaribisha uhuru kwa kusakata rhumba kwa bashasha kubwa!.

15. TITI Ashinda Ubunge Rufiji:
TITI alishinda ubunge Rufiji na kuteuliwa kuwa Waziri mdogo wa wizara ya Utamaduni na Maendeleo. Pia alishika wadhifa wa Waziri mdogo wa Afya na pia Uwaziri mdogo wizara ya Maendeleo ya Jamii. Aidha, tarehe 2.11.1962, Rais NYERERE aliagiza vyama vyote vya wanawake vivunjwe na iundwe UWT na TITI akawa ndiye Mwenyekiti.

Mwaka 1965, TITI alishindwa ubunge huko Rufiji.

16. TITI Apelekea KISWAHILI Kutumika Bungeni:
TITI alikuwa ameishia darasa la 4 tu hivyo alikuwa hawezi "kutema yai" kwa ufasaha. Siku moja mwanzoni mwa 1960s akiwa bungeni akatoa hoja kwamba wananchi wa magomeni wanataka nao wawe na taa za barabarani ambapo alisema -: "We want fire in Magomeni.... We want fire in small bottles". 

Wabunge wengi walicheka pamoja na NYERERE akiwa PM ambapo aliamuru KISWAHILI kianze kutumika bungeni.

17. TITI Alitolea nje Azimio la Arusha:

Mwaka 1967, TITI, bila kupepesa macho wala kutikisa pua, akabwaga manyanga na kujiuzulu ujumbe wa Kamati Kuu ya TANU kwani alikuwa hakubaliani na Kipengele cha 5(a) cha Azimio la Arusha kuhusu maadili kwamba ni marufuku kiongozi wa serikali au TANU kuwa na nyumba ya kupangisha.

TITI alikuwa na nyumba 2 ambapo moja aliijenga kwa kuuza vito vyake vya dhahabu na nyingine ni ya mkopo. Nyumba moja ipo Upanga mkabala na Makao Makuu, JWTZ na nyingine ipo Temeke.

Uhusiano wa NYERERE na TITI ukawa umelegalega.

18. TITI Akamatwa na Kushtakiwa kwa Uhaini:
TITI alikamatwa mwezi Octoba 1969 na kudaiwa kuwa alikula njama pamoja na OSCAR KAMBONA, GREY MATTAKA, JOHN CHIPAKA, MICHAEL KAMALIZA, WILLIAM CHACHA na ALFRED MILLINGA, kuipindua serikali. TITI alikuwa ni mwanamke pekee katika kesi hiyo.Walidaiwa kupanga kutekeleza azma hiyo wakati Rais NYERERE atakapokuwa nje ya nchi. Kesi ilianza kurindima 6.6.1970 chini ya Jaji Mkuu, Georges, CJ na upande wa mashtaka ukiongozwa na MARK BOMANI.

Kesi ilinguruma kwa siku 127. TITI  ns wenzake kasoro Bw. MILLINGS walitiwa hatiani kutokana na ushahidi madhubuti na kupewa kifungo cha maisha. TITI akaenda kutumikia kifungo gereza la Isanga, Dodoma.

19. Mume wa TITI Amwacha solemba!
Baada ya TITI kukumbwa na dhahama ya kesi ya uhaini, mmewe akaamua kumuacha kwani aliona hiyo ni fedheha kubwa isiyovumilika!.

20. Nyumba 2 za Bibi TITI Zataifishwa:
Wakati akiwa anatumikia kifungo chake cha maisha, serikali ikataifisha nyumba zake mbili zilizotajwa hapo juu.

21. MWANAMAMA Mkenya Amuomba Mwalimu Amsamehe TITI:

Mwanamama mmoja mwanasiasa machachali wa Kenya baada ya kupata habari za TITI kufungwa maisha alikuja Butiama na akaomba aonane na Mwalimu na mama yake. Alipoonana nao akasema:
"Utakuwa ni wizi wa fadhila kama wewe NYERERE utaendelea kumfunga TITI licha ya yote aliyokufanyia wewe, TZ na sehemu hii ya dunia. Tafadhali sana nimetumwa na wanawake wa Kenya nikuombe umwachie huru kama yeye alivyopigania kuachiwa huru kwa JOMO KENYATTA".

Mwalimu NYERERE alimjibu mama huyo kuwa maombi hayo ameyapokea na atayafanyia kazi.

22. TITI Achiwa kwa Msamaha wa Rais, 1972:
Rais NYERERE, akitumia mamlaka yake chini ya ibara ya 45 ya Katiba, alimsamehe TITI mwezi April 1972.

23. TITI Akwea "gogo" kuja Dsm:
Baada ya kusikia msamaha huo, TITI hakuamini maskio yake kwani aliishaamua kupambana na hali yake na alijua angefia gerezani. Hivyo, alipanda garimoshi na kuja Dsm akiwa na furaha tele na meno yote 32 nje. 

Ndugu zake walimlaki kwa bashasha na akaenda kuishi kwenye nyumba kuukuu ya mama yake iliyoko Temeke. Mama yake, aliyekuwa mtu mzima sana, almanusra azimie kwa mshtuko wa kumuona mwanae!.

24. MH. MALECELA Atumwa Kenya kuekeza TITI Yuko Huru:
Rais NYERERE alimtuma Mh. JOHN SAMWELI CIYEGWEYAMIS MALECELA , Waziri wa Mambo ya Nje, kwenda Kenya kumweleza yule mama Mwanasiasa machachali kuwa TITI ameachiwa. Baada ya kupata ujumbe huo, Mwanamama huyo aliyejawa na furaha akasema: "Naomba kamwambie Mwalimu NYERERE kwa niaba ya wanawake wote wa Kenya na wananchi wa Afrika Mashariki, nasema asante sana kwa uungwana wake".

25. TITI Aishi Maisha ya Kifukara:
Baada ya kuachiwa toka Lupango, TITI alienda kuishi Temeke. Maisha yake yalikuwa ya kipweke sana kwani ndugu na marafiki walimnyanyapaa: "Mtu angeweza kufikiri kwamba nina ugonjwa wa kuambukiza". TITI akawa muda mwingi anakaa kibarazani kwao akiuza mafuta ya taa ya rejareja ili kuweza kumudu maisha!.

26. BIBI TITI Arudishiwa nyumba zake:
Rais ALI HASSAN MWINYI alimrudishia BIBI TITI nyumba zake zote 2. Hivyo, Bibi TITI akahamia nyumba ya Upanga.

27. BIBI TITI Afariki:
BIBI TITI alifariki tarehe 5.11.2000 katika hospitali ya Net care, Afrika Kusini alikokwenda kwa matibabu.

28. BIBI TITI Apewa Mtaa, Dsm:
Kama kumbukizi ya kuheshimu mchango mkubwa wa mwanamama huyu wa kipekee, mtaa mmoja maarufu jijini Dsm umepewa jina lake "Barabara ya Bibi TITI".


MWISHO:

Huyu ndiye BIBI TITI MOHEMED, Mwanamama shupavu aliyetoa mchango mkubwa katika kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika aliyekuwa si mnafiki na hapindishi maneno kwa kile alichokiamini wala hamwogopi binadamu yeyote zaidi ya Mungu!!








No comments: