ATAKAYEDOKOA FEDHA ZA SERIKALI ATAZITAPIKA-DC MBONEKO
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko (pichani) amewataka watendaji wa serikali kutumia fedha zinazotolewa na serikali kwa malengo yaliyokusudiwa kwa kuepuka tamaa vinginevyo watakao kwenda kinyume watazitapika fedha hizo.
Mboneko ametoa kauli hiyo Februari 16,2019 wakati Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga (CCM) Mhe.Azza Hilal Hamad akitoa ufafanuzi kwa wananchi wa kata ya Usule kuhusu shilingi milioni 146.6 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu katika shule ya msingi Masunula iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Mkuu huyo wa wilaya alisema serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria watu wote watakaobanika kutumia vibaya fedha za serikali. “Msithubutu kudokoa fedha za serikali, hakuna pesa ya serikali itapotea,ukidokoa utazitapika au tutakupeleka gerezani,fedha za serikali zinapokuja zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa,mnaponunua vifaa vya ujenzi nunueni kwa bei ya jumla na siyo reja reja”,alisema Mboneko. Aidha aliwataka wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo kwani serikali pekee haiwezi kufanya kila kitu huku akisisitiza kuwa kuna maendeleo yanaletwa na serikali lakini mengine yanatokana na wananchi wenyewe.
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Azza Hilal Hamad alisema kupatikana shilingi milioni 146.6 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbili za walimu na madarasa mawili kunatokana na jitihada kubwa aliyofanya kama mbunge kuipigania shule ya Msingi Masunula ambayo imekuwa ikifanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba.
“Shule ya Msingi Masunula kwa miaka mitatu mfululizo 2016,2017 na 2018 imekuwa ikiongoza kwa shule za serikali kiwilaya na mkoa wa Shinyanga katika matokeo ya darasa la saba…baada ya kulijua hilo, mimi nilisikitika na ninasikitika sana kusikia kwamba pamoja na jitihada kubwa za walimu wanazozifanya,eti walimu hapa shuleni hawana nyumba za kuishi lakini hata vyoo tu hawana”, “Hivi hawa walimu kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa watoto wetu sisi tumeshindwa kujenga hata vyoo?,kweli ndugu zangu,kuna kitu gani hapa,yaani kabisa tunasimama tunasema shule yetu inaongoza kimkoa kwa ufaulu,kweli tuko sawa sawa kwa hili?”,alihoji Azza.
“Niliumia sana kuambiwa hakuna nyumba ya mwalimu hata mmoja,matokeo yake walimu wengine wanakaa Didia,nikaamua kulibeba na kwenda kulisemea kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alipopita Tinde,nikaiomba serikali iangalie ya msingi Masunula na kwa sababu serikali yetu ni sikivu baada ya kuomba fedha Julai 2018,serikali imetuletea fedha shilingi milioni 146.6 mwezi Januari 2019”,alisema Azza.
Mh. Azza alieleza kuwa kati ya shule zote zilizopewa fedha,Masunula ndiyo shule iliyopewa fedha nyingi kama motisha kwa sababu ya matokeo mazuri na siyo vinginevyo. “Sasa ni jukumu letu wananchi kuhakikisha kuwa fedha tulizopewa twende tukajitolee,tukafanye nguvu kazi ili tuwe na uchungu,ni jukumu letu sasa kwamba tumepewa fedha ya kujenga nyumba mbili sisi tujenge tatu,kufanya kwenu vizuri itaonesha shukrani kwa serikali”,alisema.
“Nataka tuibadilishe Masunula,tuibadilishe kata ya Usule,Masunula ifanane na yale matokeo mazuri ya mtihani wa darasa la saba yanayosomeka kule, sasa siyo matokeo mazuri halafu wazazi hamtaki kuwaunga mkono watoto wetu,kwa sababu kama watoto wapo kwenye mazingira magumu,na walimu wanafundisha kwenye mazingira magumu na mazingira ndiyo haya,tukiwaboreshea mazingira matokeo yatakuwa mazuri zaidi,si mnaweza kusikia darasa la zima limefaulu!”,aliongeza Azza.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Masunula kata ya Usule halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na kuwahimiza watendaji wa serikali na wananchi kutumia fedha zinazotolewa na serikali kwa malengo yaliyokusudiwa. Kushoto ni Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Azza Hilal Hamad (CCM). Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Masunula kata ya Usule halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Azza Hilal Hamad (CCM) akiwasisitiza wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo badala ya kusubiri serikali iwafanyie kila kitu.
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Azza Hilal Hamad (CCM) akizungumza wananchi wa kata ya Usule.
Wananchi wakimsikiliza Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Azza Hilal Hamad (CCM).
Mwananchi akiuliza swali kwa viongozi waliofika katika kata hiyo.
Wananchi wakiwa katika eneo la mkutano.
Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Azza Hilal Hamad (CCM) akikabidhi bati moja ikiwa ni sehemu ya mabati 20 aliyotoa kwa ajili ya ujenzi wa vyoo katika shule za msingi Masunula na Usule.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga,Andrew Mitumba akimshukuru mbunge Azza Hilal kwa kutoa mabati 20.
Mwenyekiti wa kijiji cha Masunula Kiyenze Majinge (kwenye nguo ya bluu) akiwaongoza Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Azza Hilal Hamad na viongozi mbalimbali kwenda kuona eneo ambapo patajengwa nyumba za walimu pamoja na madarasa katika shule ya msingi Masunula.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Masunula Gadius Kuyerwa ( wa nne kutoka kulia) akionesha na kuelezea kuhusu eneo ambapo patajengwa nyumba za walimu.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko(wa pili kulia) na diwani wa kata ya Usule, Amina Bundala wakioneshana eneo la ujenzi wa nyumba za walimu. Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
No comments: