WAMASAI SIMANJIRO WATAKIWA KUACHA KUWATUMIA WATOTO WA KIKE KAMA BIDHAA






Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile pamoja na Laigwenani wa Kimasai Mzee Maika Ngukuu (84) wakizindua Kituo cha Mtandao wa Kupambana na Ukeketaji cha Shirka la NAFGEM kilichopo Orkesumet Simanjiro mkoani Manyara.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akionesha kufuraishwa kwake na baadhi ya bidhaa za wanawake wajasiliamali wakimasai wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Mtandao wa Kupambana na Ukeketaji Orkesumet Simanjiro Mkoani Manyara .
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akipanda mti mara baada ya kuzindua Kituo cha Mtandao wa Kupambana na Ukeketaji Orkesumet Simanjiro Mkoani Manyara.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile akiwa na Wasichana waliokolewa na vitendo vya ukatili wa ukeketaji wanaopatiwa mafunzo ya ujasiliamali na Kituo cha Mtandao wa Kupambana na Ukeketaji Orkesumet Simanjiro Mkoani Manyara.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW





Na Anthony Ishengoma – Manyara


Jamii ya Wamasai nchini imetakiwa kuacha tabia ya kumtumia mtoto wa kike kama bidhaa na kuanza kuwapeleka watoto wakike shuleni badala ya kuwaozesha wakiwa wadogo kama mtaji wa kujipatia ng’ombe.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile aliyasema hayo jana alipofanya ziara ya siku moja Wilayani Simanjiro kwa aijili ya kukagua hospitali lakini pia kuzindua Kituo cha Mtandao wa Kupinga Ukeketaji kilichopo Makao Makuu ya Wilaya ya Simajiro eneo la Orkesumet.

Dkt. Ndugulile aliongeza kuwa ni muhimu kwa Wamasai kuanza kujenga jamii inayoelimika ili kuweza kutokomeza baadhi ya mila zisizofaa kwani jamii ikielimika baadhi ya mila na desturi katika jamii husika upotea zenyewe.

Awali Mkurugezi Mtendaji wa Kituo cha Mtandao wa Kupambana na Ukeketaji Simanjiro Bw. Francis Selasini alimwambia Dkt. Ndugulile kuwa kituo chake kilimwokoa mtoto wa miaka minane ambaye alikuwa anakaribia kuolewa na mzee wa miaka 72 ambaye tayari alishakubaliana na wazazi wake kumuoa na mtoto huyo kwa sasa amemaliza darasa la saba kwa msaada wa kituo hicho.

Dkt. Ndugulile aliwaambia Wazee wa Kimila kutambua kuwa ni kinyume na matakwa ya serikali na ni dhambi kubwa kuozesha watoto wadodo hususan watoto walio chini ya miaka kumi na nane akiitaka jamii hiyo kubadilika na kuelimisha watoto wa kike kwa kuzingatia usawa wa kijinsia.

Naibu Waziri Ndugulile pia amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mhandisi Zephania Chaula kuwezesha wanawake wa kimasai kiuchumi kwa kuwapatia mikopo ili waweze kuzalisha mali kama hatua ya kupambana na umasikini kwani wanaume wao mara nyingi uhama na mifugo yao na kuacha na mzigo mkubwa wa kutunza familia.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mtandao Kupambana na Ukeketaji cha NAFGEM Simajiro Bw.Francis Selasini katika ya hotuba yake kwa Naibu Waziri Ndugulile alisema wakeketaji kwa sasa wamebadili mbinu ya ukeketaji na kwasasa wanakeketa watoto wadogo kwa nyakati za husiku kwa sababu watoto hao hawana uwezo wa kutoa taarifa.

Hii hii inatokana na serikali pamoja na wadau kupinga vitendo vya ukeketaji lakini Mkurugenzi huyo pia amepinga takwimu zilizopo zinazosema mkoa wa Manyara una asilimia 58 ya vitendo vya ukatili hapa Nchini.

“Takwimu zinaonesha Mkoa wa Manyara una asilimia 58 ya vitendo vya ukatili hapa nchini lakini takwimu hizi hazioneshi uhalisia kwa kuwa Mkoa huu jamii zake zote zina mila ya ukeketaji na vitendo hivi vipo kwa wingi sana tunaomba serikali itoe njia bora ya utafiti ili tuwezo kujua kiuhalisia ukubwa wa tatizo.” Alisema Bw. Selasini.

Akihitimisha hotuba yake kituoni hapo Naibu Waziri Ndugulile aliyataka Mashirika ya SIDO, TFDA, na mengine Wilayani humo kutoa elimu ya namna bora ya kutengeneza bidhaa zenye ithibati ili bidhaa za wajasliamali wanawake ziweze kushindana kwa ubora katika Soko.

Kituo cha Mtandao wa Kupambana na Ukeketaji cha NAFGEM kilichopo Wilaya ya Simanjiro kimekuwa msaada Mkubwa kwa Jamii ya Kimasai kwani kwa sasa kinawatunza Wasichana wanaokimbia ukeketaji na kuwarudisha shuleni na wengine kuwafundisha ujasiliamali wa kutengeneza sabuni, batik na ushonaji pamoja na shule ya chekechea kwa watoto wadogo

No comments: