REVOCATUS KUULI AFUNGIWA MAISHA KUTOKUJIHUSISHA NA SOKA


Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii 

Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) imemfungia kifungo cha maisha cha kutojihusisha na Soka aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati cha Uchaguzi wa Shirikisho hilo Wakili Revocatus Kuuli. 

Hukumu hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Hamidu Mbwezeleni ambaye amezitaja sababu kubwa za kufungiwa kwa Kuuli kuwa ni kwenda kinyume na misingi ya Katiba ya TFF kwa kusambaza barua alizotumiwa na Katibu wa Shirikisho hilo Wilfred Kidao. 

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Makao Makuu ya TFF, Mbwezeleni amesema kuwa Kuuli amefungiwa kufuatia sakata la uchaguzi Simba ambapo alihojiwa kwanini ameamua kuuzuia mchakato wake kipindi unaanza na kupewa siku tatu kwa ajili ya kutoa majibu. 

Wakili hiyo alipewa siku hizo na Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Wilfred Kidao lakini hakuweza kujibu chochote na kisha baadaye kuja na majibu ya dhihaka na lugha kali kwa Kidao. Hata hivyo, Kuuli kabla hajafungiwa ilielezwa kuwa angetangaza kuachia nafasi hiyo ndani ya TFF akielezwa kukerwa kuingiliwa kwenye majukumu yake ya kazi. 

Licha ya kuuzia mchakato wa uchaguzi Simba, klabu hiyo iliendelea nao kama kawaida ambapo jana rasmi imefanikisha kufanya uchaguzi wake na kuwapata viongozi wapya. 
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF)  Hamidu Mbwezeleni akifafanua hukumu ya kifungo cha maisha cha kutojihusisha na Soka kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati cha Uchaguzi wa Shirikisho hilo Wakili Revocatus Kuuli. 

No comments: