DC awapa wiki mbili wahamiaji kuhama Kiwengwa

September 1, 2018 NA MWANAJUMA MMANGA SERIKALI ya wilaya ya Kaskazini ‘B’, imetoa wiki mbili kwa wahamiaji kutoka ya nje ya wilaya hiyo wanaoishi Kiwengwa kinyume na utaratibu kuondoka hadi pale watakapokamilisha taratibu halali za uhamiaji katika shehia hiyo. Agizo hilo amelitoa Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’, Rajab Ali Rajab alipofanya muendelezo wa operesheni maalum iliyopewa jina la ‘Safisha Kiwengwa’ kufuatia kukithiri kwa wahamiaji wanaojishughulisha na vitendo viovu ikiwemo ukahaba, ulevi, na uporaji. Alisema wameamua kufanya hivyo kufuatia kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wakaazi wa eneo hilo kulalamikia kukithiri kwa vitendo hivyo vya kihalifu hali inayowafanya kuishi kwa wasiwasi mkubwa. Alifahamisha kuwa eneo la Kiwengwa ni muhimu kwa serikali katika kuingiza pato kutokana na eneo hilo kuwa ni la kitalii, hivyo baadhi ya vitendo vinavyojitokeza vinasababisha kuvurugika kwa mmong’onyoko wa maadili. Hata hivyo, Rajab ambae pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo alisema zaidi ya watu 50 wamekamatwa katika operesheni hiyo, huku akiahidi kamati hiyo itaendeleza zoezi hilo ili kumaliza vitendo hivyo na kurudisha haiba ya watu wa Kiwengwa. Aidha alisema anakusudia kufanya operesheni maalum kwa lengo la kudhibiti vijana na watu wa kabila la wamasai ambao mara nyingi wamekuwa wakifanya vurugu wakiwa wanatembea na silaha za jadi. Nae Katibu Sheha wa shehia hiyo, Vuai Juma Kondo amekiri kuwepo kwa wahamiaji wasiofuata taratibu za kiuhamiaji na kusababisha usumbufu kwa uongozi wa shehia pindi wanapopatwa na matatizo. Zanzibarleo

The post DC awapa wiki mbili wahamiaji kuhama Kiwengwa appeared first on Mzalendo.net.

No comments: